Simba, Namungo kula viporo Februari 4
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa taarifa ya kurejea kwa Ligi Kuu Bara baada ya kusimama kupisha michuano ya Mapinduzi Cup na Chan yanayoendelea nchini Cameroon.
TPBL imeeleza mechi za mzunguko wa 19 zitaendelea kuanzia Februari 13 huku zile za viporo zikianza Februari 4 vilivyotokana na timu za Namungo na Simba kushiriki mashindano ya CAF.
"Mechi zilioahirishwa kwa baadhi ya timu kuwa kwenye mashindano ya CAF zinatarajiwa kuanza kuchezwa Februari 4 kabla ya kuanza kuchezwa mzunguko wa 19 Februari 13," imeeleza taarifa hiyo.
Simba ipo nafasi ya pili na wana alama 35 kwenye msimamo wa Ligi imecheza mechi 15 na ina viporo vya mechi dhidi ya Azam, Dodoma Jiji na Namungo wenyewe.
Tayari timu hiyo imefanya usajili wa wachezaji wawili akiwemo Perfect Chikwende toka Zimbabwe na kiungo mkabaji Doxa Gikanji kutoka DR Congo.
Kwa upande wa Namungo wao wana viporo vinne ambavyo ni dhidi ya Gwambina, Ruvu Shooting, Simba na KMC.