Simba kwa mziki huu patachimbika

DROO ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ilipangwa wiki iliyopita huko Cairo, Misri ambapo wawakilishi wa Tanzania, Simba waliangukia kundi A lenye timu za Al Ahly, AS Vita na El Merrikh.

Timu mbili zitakazoongoza kundi zitafuzu robo fainali ya mashindano hayo. Mwanaspoti linakuletea tathmini ya timu tatu zitakazokutana na Simba.

AL AHLY

Timu ya Al Ahly ilianzishwa 1907 na inaelekea kutimiza miaka 114 na ni sehemu ya timu za michezo mbalimbali zilizopo chini ya klabu ya Al Ahly - mingine ikiwa ni kikapu na wavu. Inautumia Uwanja wa Taifa wa Misri unaoingiza watu 70,000 na pia ule wa Al Ahly unaoingiza 30,000.

MAFANIKIO

Ligi Ya Mabingwa Afrika hakuna namna utaacha kuizungumzia Al Ahly kwani ndio timu yenye mafanikio makubwa zaidi kuliko nyingine yoyote. Ni timu iliyotwaa mara nyingi taji hilo ikifanya hivyo mara tisa, huku ikimaliza ikiwa nafasi ya pili mara nne. Imetwaa Super Cup mara tano na Kombe la Shirikisho Afrika mara moja. Al Ahly ndio timu yenye mafanikio zaidi duniani kwani imetwaa mataji 90 ya mashindano tofauti.

THAMANI & KIKOSI

Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com kikosi cha Al Ahly kina thamani ya Euro 27.25 milioni (Sh77.2 bilioni) na mchezaji mwenye thamani kubwa ni kipa na nahodha wao, Mohamed El Shenawy - Euro 2.5 milioni (Sh 7.1 bilioni). Kocha wao ni Pitso Mosimane, raia wa Afrika Kusini aliyetwaa taji hilo mara mbili, moja akiwa na timu hiyo na jingine akiwa na Mamelodi Sundowns. Nyota wa kuchungwa Al Ahly ni Shenawy; mabeki Ayman Ashraf, Rami Rabia, Saad Samir na Ali Maaloul wakati viungo ni Aliou Dieng, Karim Nedved, Walid Soliman na Hussein El Shahat huku mastraika ni Salah Mohsen, Aliou Badji, Junior Ajayi na Walter Bwalya.

REKODI V SIMBA

Haitakuwa mara ya kwanza Simba kuumana na Al Ahly katika mashindano ya kimataifa kwani walikutana mara nne ambapo kati ya hizo, kila moja imeshinda mara mbili. 1985 walikutana Kombe la Washindi ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 nyumbani na ikafungwa 2-0 ugenini.

Mwaka 2019 walikutana kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa na mechi ya awali huko Misri, Al Ahly ilishinda 5-0 na Simba ikashinda 1-0 nyumbani.

AS VITA

Ni timu kongwe nchini DR Congo ikiwa na miaka 85 kwani ilianzishwa 1935 kama ilivyo Yanga, mwaka mmoja kabla ya kuanzishwa kwa Simba. Inatumiwa Uwanja wa Martyrs de la Pentecôte uliopo Kinshasa unaoingiza takribani mashabiki 125,000 ukiwa na eneo la kuchezea lenye nyasi za asili.

MAFANIKIO

Hufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na mafanikio ya juu waliyoyapata ni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa 1973, kuingia fainali mara mbili, moja kwenye mashindano hayo na nyingine Kombe la Shirikisho Afrika.

Imewahi kutinga nusu fainali ya klabu Afrika mara kadhaa na pia robo fainali na kwa hatua ya makundi imekuwa ni kama utamaduni wao.

THAMANI & KIKOSI

AS Vita inanolewa na Florent Ibenge anayeinoa pia timu ya Taifa ya DR Congo na inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali.

Wachezaji wa kuchungwa ni washambuliaji Ricky Tulengi na Fiston Mayele; mabeki Djuma Shabani, Ousmane Ouattara na Patou Ebunga Simbi na viungo Merveille Kikasa Wamba na Sidi Yacoub

REKODI v SIMBA

Timu hizo zimeshakutana mara nne tofauti na AS Vita imefanya vizuri zaidi kwani kati ya hizo imeshinda mara tatu na kufungwa moja. Walikutana ya kwanza 1978 Klabu Bingwa Afrika ambapo Vita walishinda 1-0 mechi zote nyumbani na ugenini. Mwaka 2019 walikutana hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ambapo AS Vita walishinda 5-0 nyumbani na Simba ikashinda 2-1 hapa Tanzania.

AL MERREIKH

Ilianzishwa Novemba 14, 1927 mjini wa Omdurman na inatumia Uwanja wa Omdurman unaoingiza watu 43,000 na jina la utani ni Mashetani Wekundu.

MAFANIKIO

Al Merrikh imetwaa Kombe la Washindi Barani Afrika 1989 na imewahi kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2007. Katika Ligi ya Mabingwa Afrika mafanikio makubwa ni kutinga nusu fainali ya mashindano hayo 2015 na pia imewahi kutinga robo fainali na makundi mara nyingi.

THAMANI & KIKOSI

Kwa mujibu wa mtandao wa www.tyransfermarkt.com, thamani ya kikosi ni zaidi ya Sh5 bilioni. Timu hiyo inanolewa na Didier Gomes Da Rosa, raia wa Ufaransa na Ureno.

Wachezaji wa kuchungwa ni Saifeldin Malik Bakhit, Emad Elsin, Bakr Al Madina, Dhiya Musa, Alsamany Alsaw na Wendi Panga.

REKODI V SIMBA

El Merrikh watakuwa na kibarua cha kumaliza unyonge dhidi ya Simba kwani hawajawahi kuonja ushindi pindi wakutanapo na wawakilishi hao wa Tanzania.

Wamekutana mara tatu na zote hizo Simba wameibuka na ushindi. Mara ya kwanza katika Klabu Bingwa 1994 na Simba wakashinda 1-0 katika kila mechi nyumbani na ugenini. Mwaka 2011 walikutana nusu fainali ya Kombe la Kagame na Simba wakashinda kwa penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1.

MDAU

Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Phillip Alando anasema: “Ni kundi gumu kwa majina ya timu zilizopo ila sidhani kama baadhi ya timu zina ule ubora ule wa zamani, mfano Al Merrikh na Vita Club.”