Simba kama Ulaya

ACHANA na ambavyo wanaishi kishua wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Simba kwenye hoteli ya nyota tano Mercure hapa Ismailia Misri iliyopo pembezoni mwa fukwe ya bahari.
Katika mazoezi ya jana asubuhi wachezaji wa Simba wote waliwekewa vifaa maalumu vya kuvaa kwenye mwili wao kama kawoshi (Vest), ili kuonyesha ufanisi wao wa kazi uwanjani kwenye mazoezi hayo.
Kifaa hicho kilivyo kama GPRS, kilikuwa na kazi maalumu ya kuonyesha kila mchezaji uwezo wake wa kukimbia, utimamu wake wa mwili, hali yake ya kiafya, mapigo ya moyo, amekimbia umbali gani uwanjani, amekimbia eneo gani na mambo mengine ya msingi.
Dhumuni la kifaa hicho ilikuwa ni kuonyesha kila mchezaji uwezo wake ni upi kwenye mambo hayo ya msingi na kila mmoja alionekana kufikia kile alichokuwa anahitaji kocha, Zoran Maki.
Katika hatua nyingine kwenye mazoezi ya asubuhi kulikuwa na vifaa vingine vya maana kama midoli maalumu kama watu, midoli mingine ya plastiki iliyotumika kwenye mazoezi ya faulo, koni maalumu ndefu na fupi, maputo ya kukimbilia na mipira maalumu.
Ukiachana na vifaa hivyo, wachezaji wa Simba walifanya mazoezi aina nne tofauti na yalikuwa yakisimakiwa na makocha wote watatu kila mmoja akiwa na eneo lake.
Zoezi la kwanza wachezaji walikwenda kukimbia bechi iliyopo pembezoni mwa uwanja, baada ya hapo walikuja kufanya mazoezi ya viungo kisha kwenda kwenye yale ya mbinu.
Kocha wa viungo, Sbai alikuwa akisimamia zoezi hilo la bechi na kumtaka kila mchezaji kukimbia mbio ndefu na fupi kwenye eneo hilo lililokuwa na mchanga mwingi.
Baada ya hapo Sbai na Kocha msaidizi, Selemani Matola wote walikwenda kusimamia mazoezi ya viungo yaliyofanyika katika mwa uwanja katika eneo la kuchezea na hapo ndio vilitumika vifaa vingi zaidi.
Zoran na wasaidizi wake hao wawili walisimamia shoo ya zoezi la mwisho la kufunga ambalo lilikuwa na njia tatu tofauti huku nyota wote wa mbele walionekana kuwa moto.
Njia ya kwanza ilikuwa kushambulia kupitia pembeni na mabeki, kisha likafuata kushambulia kati viungo walitengeneza nafasi kwa washambuliaji na nyingine ilikuwa kushambulia kwa kushtukiza.
Katika zoezi hilo la kufunga, Augustine Okrah, Clatous Chama, John Bocco, Pape Sakho, Pater Banda na Moses Phiri walikuwa kwenye viwango bora kwa kufunga mabao ya maana wakiwatesa makipa, Ally Salim na Benno Kakolanya.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kila zoezi lililokuwa likiendelea hapo ni kuhakikisha wanakwenda kutumia kwenye mechi zao za msimu ujao na kuhakikisha wanafanya vizuri.
“Timu inaendelea kuimarika kulingana na aina ya mazoezi ya kila siku na naimani tutakuwa na kikosi bora zaidi msimu ujao na kufanya vizuri katika mashindano ya ndani,” alisema Rweyemamu.