Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba hii ni hapa tu!, tia Onyango, weka Okwa

MPANGO wa Simba kumsajili Cesar Manzoki umesubirishwa kidogo, lakini ufanisi wa kikosi chake katika mechi sita ilizocheza tangu siku ya kilele cha Tamasha la Simba Day, unawapa nguvu ya kutoyumba kwa safu yake ya ushambuliaji hadi pale dirisha dogo litakapofunguliwa Desemba.
Ilitegemewa Manzoki atue Simba katika usajili wa dirisha kubwa uliofungwa majuzi saa 6.00 usiku lakini vinara hao wa Ligi Kuu Bara waliwekewa ngumu na Vipers iliyokuwa ikimmiliki mchezaji huyo kabla ya kuamua kumuuza huko China katika klabu ya Dalian kwa mkataba wa miezi minne.
Lakini licha ya kutokuwepo Manzoki, Simba imeonekana inaweza kupambana na ratiba iliyo mbele yake kwa kipindi cha miezi mitatu na nusu iliyobakia hadi wakati wa dirisha dogo ili kuona kama inaweza kumsajili baada ya kumpa mkataba wa awali kwenye dirisha lililofungwa.
Tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini maeneo kadhaa yanayoipa uimara Simba kwa sasa ingawa pia kuna madhaifu kadhaa ambayo inapaswa kuyafanyia kazi kutegemeana na kile ilichokionyesha katika mechi sita ilizocheza kuanzia ile ya siku ya kilele cha Simba Day dhidi ya St. George hadi ya mwisho ya kirafiki waliyocheza na Al Hilal ya Sudan.


UBABE UPO HAPA
Kwa siku chache ambazo ameinoa Simba, kocha Zoran Maki ameonekana kugawanya jukumu la ufungaji mabao kwa wachezaji wa nafasi tofauti na sio kutegemea ile ya mshambuliaji wa kati tu.
Ni kama ilivyokuwa wakati wa kocha Sven Vandenbroeck ambapo mawinga na viungo washambuliaji wa Simba walichangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mabao kwa timu hiyo.
Katika mechi sita ilizocheza kuanzia siku ya Simba Day hadi sasa, Simba imefunga jumla ya mabao 12 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo ambayo kati ya hayo, moja tu limefungwa na mshambuliaji wa kati, matano yakifungwa na viungo washambuliaji huku mabao sita yakipachikwa na mawinga.
Zoran ameonekana kuwapa uhuru zaidi mawinga wake kuingia ndani ya uwanja na kulisogelea lango la timu pinzani jambo ambalo limewafanya wawe wanapata nafasi za kufunga mara kwa mara.
Ukiondoa uimara katika eneo hilo, kocha huyo pia ameonekana kuifanya Simba kucheza soka la kasi na kutokaa na mpira kwa muda mrefu kwa wachezaji wake hasa wanapoelekea kushambulia.
Hilo limeifanya Simba chini yake kufungua mianya na kutengeneza nafasi nyingi kutokana na kuchelewa kwa wapinzani kujipanga lakini pia wananufaika kwa kuwa na namba kubwa ya wachezaji pindi wanaposhambulia au hata pale wanapozuia.
Simba pia ina uimara katika uzuiaji wa mipira ya juu ambayo ilionekana kuwapa changamoto kubwa katika msimu uliopita na kuwafanya waruhusu mara kwa mara mabao yatokanayo na aina hiyo ya mashambulizi.
Ujio wa beki Mohamed Ouattara ambaye anacheza sambamba na Enock Inonga ambao wote ni warefu kimaumbo, umekuwa na msaada mkubwa kwa Simba katika kushughulika na mashambulizi yatokanayo na mipira ya juu.


TATIZO LIPO HAPA
Mbali na uimara huo, Simba imeonekana kuwa na udhaifu katika baadhi ya mambo ndani ya uwanja ambayo kocha Zoran Maki anapaswa kuyafanyia kazi ili timu yake iwe tishio zaidi.
Kumekuwa na udhaifu wa kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri baina ya walinzi wake wawili wa kati, Inonga na Ouattara jambo ambalo limechangia nyakati kadhaa wategeane katika kudhibiti washambuliaji wa timu pinzani na kuifanya Simba baadhi ya nyakati uruhusu mabao au lango lao kuwa kwenye misukosuko kutokana na makosa yao.
Pia wawili hao wameonekana kutokuwa na kasi kasoro ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu kwa kujikuta wakiachwa mara kwa mara na washambuliaji wenye kasi na wanyumbulifu au wakati mwingine kupelekea kufanya faulo ambazo huwa na faida kwa timu pinzani.
Udhaifu mwingine ambao unaipa wakati mgumu Simba upo katika nafasi ya kiungo mkabaji ambapo waliopo wanaonekana kutoilinda vyema safu yao ya ulinzi na kuachia mianya ambayo nyakati kadhaa hutumiwa na wapinzani kuwashambulia kirahisi.
Washambuliaji wa kati wa Simba waliopo hivi sasa wamekuwa na udhaifu pia wa kuchelewa kujipanga katika nafasi sahihi na kutotulia katika nafasi stahiki pindi wanapokuwa wanashambulia jambo ambalo limekuwa likiwapa uhuru walinzi wa timu pinzani kuwadhibiti na kuichelewesha timu kupata mabao.


WASIKIE WADAU
Akikizungumzia kikosi hicho, nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema: "Kitu ambacho kimeongezeka benchi la ufundi limefanyia kazi matatizo ya msimu uliopita yaliyokuwa ni kupeleka mpira eneo la ushambuliaji.
Alisema kina Nelson Okwa, Augustine Okrah, Pape Sakho wameongeza kitu na mikimbio ni mingi eneo la mbele na wamemuamsha Chama aliyerejea kwenye kikosi.
Kwa upande wa kikosi, Mayay alimpanga Aishi Manula langoni, huku mabeki wanne akiwaweka Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Kennedy Juma na Henock Inonga.
Viungo aliwapanga Sadio Kanoute, Clatous Chama, Okrah na Sakho na mbele kuwapa nafasi Moses Phiri na Habib Kyombo.
Kocha na Mchambuzi Ibrahim Masoud 'Maestro', alisema Simba kuwa na tatizo maeneo kadhaa ikiwemo beki wa kati na kutokuwa na balansi ya eneo la kiungo na ushambuliaji.
"Wachezaji wengi wa Simba vipaji vyao vinazidiana kidogo kidogo, lakini eneo la ulinzi limekuwa tatizo kwa Simba muda mrefu ila ujio wa Ouattara unaweza kuongeza kitu kutokana na ubora na uzoefu wake," alisema Maestro ambaye kitaaluma ni kocha aliyesimamia Kamati ya Ufundi ya Simba misimu kadhaa iliyopita na kuongeza;
"Kingine timu ina wachezaji wengi wenye sifa zinazofanana eneo la kiungo jambo linaloweza kuifanya timu ikose kuwa na mizani sawa katika maeneo mengine na pia shida nyingine inayoweza kutokea ni kwa katika machaguo ya kocha amtumie nani kwenye mechi ipi na anahitaji kuwa na msoma mchezo aliye makini sana ili kuepusha migongano ya hapa na pale."
Juu ya kikosi, Maestro alisema angemtumia Inonga kama namba sita huku mabeki wakiwa Zimbwe, Kapombe, Ouattara na Onyango na langoni atakuwepo Manula.
Viungo wengine watakuwa Kanoute, Chama na Okwa huku Sakho na Okrah wakicheza kama mawinga na washambuliaji akaweka Bocco na Phiri.
Mchambuzi nguli wa gazeti hili, Edo Kumwembe yeye alisema; "Katika mechi hizi za mwanzo bado Simba hawajaonyesha utawala mkubwa uwanjani kwa maana hawajaweza kutawala mchezo kwa muda mwingi jambo ambalo timu kubwa zinafanya.
Lakini hiyo sio shida kubwa kwani inatokana na wachezaji wengi kuwa wapya nadhani baada ya mechi mbili za kimataifa watakuwa imara zaidi," alisema Edo.
Alipohitajika kutaja kikosi cha kwanza cha Simba, kwa upande wake aliweka wazi anaweza kupanga hadi eneo la beki wa kati tu kwa maana ya Manula, Kapombe, Zimbwe, Ouattara na Inonga lakini kuanzia kiungo hadi mbele hajapata watu wa moja kwa moja kama ilivyo kwa kocha Zoran anayebadili badili wachezaji.
Nyota wa zamani wa timu hiyo, Mussa Mgosi ambaye kwa sasa ni kocha wa timu za vijana Simba alisema kikosi kimekamilika kwani usajili umefanyika kwa malengo.
"Kilichobaki ni wachezaji kujua nini Simba inataka kutoka kwao kisha wapambane kuhakikisha kinatimia lakini kiujumla timu ni nzuri na inaweza kufika mbali zaidi kimataifa," alisema Mgosi aliyekataa kutaja kikosi chake kama angekuwa kocha akidai kwa sasa yupo ndani ya Simba na akifanya hivyo atakuwa anamuingilia kocha mkuu.
Mchezaji wa zamani wa Simba ambaye ni kocha kwa sasa Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema; "Watu wana haraka na wanataka matokeo ya hapo hapo, Simba imesajili wachezaji wengi hivyo wanahitaji muda wa kutosha ili kuelewana vizuri.
"Kwa sasa siwezi kupanga kikosi moja kwa moja kwasababu wachezaji wengi ni wapya lakini kuna waliokuwepo kama Manula, Kapombe, Zimbwe, Inonga na yule mpya (Ouattara) wanafaa kucheza eneo la ulinzi na kwenye kiungo Mkude na Chama wanastahili kucheza," alisema Julio.
Kocha Kennedy Mwaisabula yeye alieleza Simba kusumbuliwa na maeneo mawili ambayo ni beki wa kati na mshambuliaji wa kati jambo ambalo kocha anahitaji kuwa nalo makini.
"Inahitaji umakini zaidi kwenye beki wa kati, Ouattara na Inonga wote wanafanana si sawa kucheza pamoja wanahitaji mtu mtulivu zaidi kama Erasto Nyoni akiwa kwenye ubora wake.
Eneo la straika hawajawa na mtu wa uhakika kama ilivyokuwa kwa kina Mugalu na Kagere hivyo kocha anapaswa kuliangalia vyema pia eneo lile," alisema Mwaisabula aliyetaja kikosi chake cha kwanza kwa sasa kuwa; Manula, Kapombe, Zimbwe, Inonga, Ouattara, Mkude, Sakho, Mzamiru, Kibu, Chama na Okrah.