Simba hii mtaitaka lawama

Mchezo huo ulishuhudiwa na maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo.
Muktasari:
- Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Joseph Omog kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuweka kambi kwa mwezi mmoja mjini Morogoro, ambako alikuwa akiwafua vilivyo nyota hao na kucheza mechi kadhaa.
SIMBA imerudi upya, asikuambie mtu. Wapinzani wao wa Ligi Kuu Bara lazima wajipange kwelikweli kwani, hakuna namna nyingine wa kuidhibiti. Jana Jumatatu ilikuwa ikiadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa kwake, ikatambulisha kikosi chake kipya cha msimu huu, lakini pia ikapepetana na AFC Leopards ya Kenya.
Unajua kilichotokea. Katika tamasha hilo la Simba Day lililopambwa na burudani mbalimbali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba katika ubora wake, ilinguruma kwa kuichakaza ‘Ingwe’ kwa mabao 4-0, huku Laudit Mavugo alithibitisha kuwa, kweli yeye ni mfalme mpya Msimbazi kwa kufunga moja na kuhusika na mabao mengine mawili.
Shiza Kichuya aliyepiga mpira mwingi na kushangiliwa mno uwanjani hapo, alitupia moja na mengine mawili yakiwekwa kimiani na Ibrahim Ajib.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Joseph Omog kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuweka kambi kwa mwezi mmoja mjini Morogoro, ambako alikuwa akiwafua vilivyo nyota hao na kucheza mechi kadhaa.
Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo, ilimchukua Ajib dakika 38 kupiga shuti la umbali mrefu ‘mwendokasi’ ambalo lilimshinda kipa wa Leopards, Ian Otieno na kutinga wavuni.
Ajibu aliifungia Simba bao la pili dakika ya 57 akiunganisha kazi nzuri ya Kichuya, ambaye dakika 10 baadaye alifunga bao la tatu. Mavugo alifanya kazi nzuri ya kuwatengenezea washambuliaji hao mabao mawili ya mwisho.
Mavugo na Kichuya waliibuka kuwa nyota wa sherehe hiyo baada ya kupiga mpira mwingi ambapo, kila wakati walikuwa wakiwanyanyasa mabeki wa Ingwe.
Katika mchezo huo wachezaji watano wapya walifanikiwa kuanza ambao ni mabeki Javier Bokungu na Method Mwanjali, viungo Mussa Ndusha na Shiza Kichuya pamoja na straika Muivory Coast, Blagnon Frederick. Nyota wengine wapya, Mdhamiru Yassin, Jamal Mnyate na Mavugo waliingia katika kipindi cha pili. Viungo Ndusha na mabeki Mwanjali walionyesha uwezo mkubwa.
Kocha Omog aliendelea kutumia mfumo wa viungo watatu ambapo, katika eneo la kati walikuwepo Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto pamoja na Ndusha katika kipindi cha kwanza na kipindi cha pili Mdhamiru aliingia kuchukua nafasi ya Kazimoto.
Mo atia timu
Bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye ametangaza nia ya kuwekeza Simba na kuungwa mkono na wanachama wa klabu hiyo, alitia timu uwanjani na kushangiliwa na maelfu ya mashabiki wa timu hiyo waliofurika kuongeza msisimko wa mchezo huo.
MO aliambatana na mgeni rasmi, Paul Makonda pamoja na viongozi wa Simba kwenda kusalimiana na wachezaji wa timu zote kabla ya kuanza kwa mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki.
Kichuya azua tafrani
Katika hali isiyotarajiwa, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliwatambulisha wachezaji wote na kuwasahau Shiza Kichuya pamoja na nahodha, Mussa Hassan ‘Mgosi’ jambo ambalo lilizua taharuki kwa mashabiki ambao, walisimama na kuanza kuhoji alipo nyota huyo ambaye wamekuwa wakiambiwa amejiunga na Simba.
Baada ya dakika chache Manara alidai alifanya kitendo hicho kwa makusudi na kumtambulisha rasmi Kichuya ambaye, alipokelewa kwa shangwe na vifijo ambapo baadaye alipiga mpira mwingi uliowafanya mashabiki wa Simba waliokuwepo uwanjani hapo kusema ‘Wallah, hatujawahi kuona utamu kama huu”.
Simba, Yanga watifuana
Kabla ya kuanza kwa mchezo huo mashabiki wa Simba walienda na kutaka kukaa katika jukwaa la upande wa kulia ambalo hukaliwa na mahasimu wao, Yanga jambo lililosababisha sintofahamu na kurushiana maneno ya hapa na pale.
Hata hivyo, baadaye mashabiki wa Yanga walilazimika kuketi katika eneo dogo na kuwapisha wenzao wa Simba ambao, walikuwa na jeuri kubwa kwa kudai kuwa sherehe ni yao na ‘haikodishwi’.
Kiongera ashangiliwa
Straika wa zamani wa Simba, Raphael Kiongera alirejea nchini kwa mara ya kwanza tangu alipoachwa na timu hiyo ambapo, alikuwa na kikosi cha Ingwe lakini alijikuta akishangiliwa na mashabiki wa Simba ambao bado walionyesha kuwa na imani naye.
Kiongera baadaye aliongoza safu ya mashambulizi ya Ingwe na katika kipindi cha kwanza kipa Vincent Angban, alilazimika kutumia uzoefu kuzuia mashambulizi yake mawili.
Mashabiki lukuki
Nani amekwambia kuwa Simba ina mashabiki wachache? Katika sherehe hizo za Simba Day maelfu ya mashabiki walijitokeza uwanjani hapo na kujaza karibu robo tatu ya uwanja. Makadirio ya awali yalionyesha mashabiki zaidi ya 35,000 waliingia uwanjani kutazama mchezo huo.
Katika sherehe hiyo kulikuwa na ukatwaji wa keki ambapo viongozi waandamizi wa klabu hiyo na wale wa sasa walijumuika kuitafuna sambamba wageni wengine huku bendi ya Twanga Pepeta chini ya Khalid Chokoraa ikimwaga burudani ya kutosha.