Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba eeh bwana ndio

MSIMU uliopita Wekundu wa Msimbazi hawakuwa na raha kutokana na watani zao Yanga kuonekana kuwa wazuri, wakizoa mataji yote kuanzia Ngao ya Hisani, Kombe la FA na Ligi Kuu Bara.

Yanga ilitamba kwa kuwa ilikuwa na kikosi kipana na imara kilichoongozwa na wapachika mabao matata, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Malimi Busungu.

Lakini safari hii imepiga hesabu kali na kufanya jambo ambalo kila shabiki wa klabu hiyo lazima achekelee kwa kutambua kuwa, dawa ya kumfunga mdomo Jerry Muro, yule Msemaji wa Yanga aliye kifungoni imepatikana.

Unajua ni nini? Usajili wa straika Laudit Mavugo katika kikosi hicho umeifanya Simba kupata kombinesheni sita tofauti za wapachika mabao na kuwazidi kete watani zao Yanga ambao mpaka sasa wana kombinesheni nne tu za maana.

Mavugo anaungana na washambuliaji wengine, Ibrahim Ajib, Blagnon Frederick, Danny Lyanga, Ame Ali na Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambao wanatengeneza pacha hizo sita hatari za mabao ingawa kuna habari kwamba Mgosi anastaafu.

MBILI TU MATATA

Yanga kwa sasa ina washambuliaji wa kati watano; ambao ni Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe, Malimi Busungu pamoja na Mateo Anthony.

Kocha wa Simba, Joseph Omog tayari amejaribu kombinesheni mbili tofauti ambazo zimeonekana kuzaa matunda, huku akisaliwa na kombinesheni nyingine kama tano hivi ambazo bado hazijatumika.

Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya AFC Leopards, Omog alianza kwa kuwajaribu Blagnon Frederic na Ibrahim Ajib ambao walifanya vizuri kabla ya baadaye kubadilisha na kumchezesha Ajib na Mavugo ambao walionekana kuivana.

Mbali na kombinesheni hizo mbili, Simba bado ina wigo mpana wa kuwachezesha Blagnon na Mavugo, Danny Lyanga na Mavugo, Mgosi na Mavugo, Ajib na Lyanga pamoja na Ame Ali na Mavugo ama Blagnon jambo ambalo linawafanya wawaache mbali watani zao wa Jangwani.

JANGWANI NAKO

Kwa upande wa Yanga mpaka sasa wana kombinesheni nne tu tofauti za mabao ambazo ni ile ya Ngoma na Tambwe iliyofanya vizuri msimu uliopita huku kocha Hans Van Der Pluijm akijaribu kutengeneza kombinesheni mpya ya Obrey Chirwa na Ngoma.

Yanga bado ina kombinesheni nyingine mbili ambazo zinaweza kufanya kazi kwa ufanisi ambazo ni Tambwe na Chirwa na ile ya Ngoma na Busungu.

Nyota wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema timu hiyo kwa sasa ina safu imara ya ushambuliaji ambayo bila mashaka inaweza kupambana kuwania taji la Ligi Kuu Bara na lile la FA.

“Kocha ana chaguo pana katika eneo la ushambuliaji, ana watu ambao wana uwezo mkubwa na wanaweza kupata matokeo kwa wakati wowote, nadhani safu hii inatosha kwenda kwenye mashindano,” alisema Ulimboka.

“Siyo katika washambuliaji wa kati pekee, hata kwa washambuliaji wa pembeni kama Shiza Kichuya na Jamal Mnyate wako vizuri, kikubwa ni kwamba usajili wa mwaka huu uko imara,” alifafanua.