Simba chupuchupu, mwamuzi awa gumzo KMC Complex

Muktasari:
- Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi 60 na sasa ikihitaji tatu tu kuweza kuungana na Yanga iliyokata tiketi ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.
SIMBA imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa katika mechi iliyojaa matukio ya utata ikiwamo refa Kefa Kayombo kutoka Mbeya kuweka rekodi ya kuongeza dakika 15 ikiwa ni muda mrefu katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku Wekundu hao wakisaliwa na dakika 90 kukata tiketi ya CAF.
Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi 60 na sasa ikihitaji tatu tu kuweza kuungana na Yanga iliyokata tiketi ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.
Katika mchezo huo, Simba ilisubiri hadi dakika ya 90’+19 kupata bao la ushindi baada ya Mashujaa iliyomaliza pungufu baada ya kipa Patrick Munthary kulimwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu, dakika 80, huku Leonel Ateba akifunga mabao yote mawili kwa njia ya penalti na kufikisha mabao 10.
Hadi kipa huyo mwenye clean sheet 12 akitolewa uwanjani matokeo yalikuwa bao 1-1 na Mashujaa kulazimika kumtumia mchezaji wa ndani Abdulnassir Gamal langoni kutokana na kumaliza idadi ya wachezaji wa kuwabadilisha, ikilingana na tukio la mechi ya Simba dhidi ya Fountain Gate iliyoisha kwa sare ya 1-1 baada ya kipa John Noble kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kuchelewesha muda kwenye mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.
Katika mchezo huo, dakika 45 za kipindi cha kwanza, Mashujaa ilionekana kucheza kwa nidhamu kubwa katika safu yao ya ulinzi, ikiongozwa na Baraka Mtuwi na Abdulmalik Zakaria.
Licha ya kuwa na umiliki mkubwa wa mchezo, Mashujaa ilionekana kuwa na namba kubwa ya wachezaji kwenye eneo lao jambo ambalo liliwapa wakati mgumu, Ellie Mpanzu, Edwin Balua na Awesu Awesu kufungua ngome yao.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Mashujaa kuwa mbele kwa bao 1-0. Simba ilirejea kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko matatu kwa mpigo.
Kocha, Fadlu Davids aliamua kuwatoa Nouma, Duchu na Balua huku nafasi zao wakiingia Kibu, Kapombe na Tshabalala.
Mabadiliko hayo yalionekana kuongeza kitu kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba na Kibu alionekana kuongeza ubunifu na dakika chache baadae mambo yalijipa kwa Simba kupata bao la kusawazisha.
Dakika ya 65, Simba ilisawazisha kwa mkwaju wa penalti kupitia Leonel Ateba ambaye alifunga bao lake la tisa msimu huu sawa na mshambuliaji mwenzake, Steven Mukwala.
Wakati mzani ukiwa sawa katika dakika ya 80, Mashujaa iliwalazimu kucheza pungufu baada ya kipa wao, Patrick Munthary kuonyeshwa kadi ya pili ya njano ambayo iliambana na nyekundu.
Munthary alipata kadi hiyo ya pili ya njano baada ya kuonekana kumtupia maneno mwamuzi wa mchezo huo, Kefa Kayombo wakati ambao Simba ilipata kona.
Mashujaa kwa kuwa ilimaliza idadi ya kufanya mabadiliko iliwabidi mchezaji wao mmoja wa ndani Jamal kukaa golini.
Baada ya kuwa pungufu, Mashujaa iliamua kucheza kwenye eneo lao kwa ajili ya kuambulia walau pointi moja kwenye mchezo huo mpango ambao ulioenakana kufanya kazi vizuri katika dakika zilizosalia.
Simba ilipata bao la ushindi katika dakika 90+19 baada ya Kapombe kuangushwa eneo la hatari la Mashujaa na mwamuzi kuipa Simba mkwaju wa penalti ambao ulifungwa na Ateba.