Simba balaa Afrika, Mgunda asema na bado

HUYU Phiri anajua sana. Ndivyo mashabiki wa Simba juzi Jumapili walivyotamba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya Mzambia huyo kufunga mara mbili na kuizamisha Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa mabao 2-0.

Phiri aliyesajiliwa msimu huu kutoka Zanaco ya Zambia, alifunga mabao hayo moja kila kipindi na kuivusha Simba kwenda raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. kwa jumla ya mabao 4-0, baada ya awali kufunga 2-0 ugenini, huku Phiri alifunga pia bao.

Simba sasa itavaana na kati ya Red Arrows ya Zambia au Premiero do Agosto ya Angola ambazo wakati tukienda mitamboni zilikuwa uwanjani zikipepetana kwenye mchezo wa marudiano, nchini Angola.

Ikicheza kwa mara nyingine chini ya kocha wa mpito, Juma Mgunda, Simba iliupiga mpira mwingi na kuwapa furaha mashabiki wa wao walijazana Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mgunda alimuanzisha beki Israel Mwenda na Augustine Okrah, huku akiwapiga benchi Pape Ousmane Sakho na Mohammed Ouattara na Mkenya Joash Onyango na Shomary Kapombe wakiwa jukwaani katika mechi hiyo kali.

Okrah alishirikiana vyema pamoja na Clatous Chama, Phiri na Kibu Denis katika eneo la ushambuliaji waliitesa ngome ya wageni.

Simba iliuanza mchezo kwa kasi ikisaka bao na dakika ya pili tu iliifika langoni mwa Big Bullets kwa pasi ya Chama kumkuta Mzamiru Yassin lakini shuti lake linatoka nje kidogo.

Kasi ya Simba iliwafanya wageni wafanye mabadiliko dakika ya 24 kwa kumtoa Alick Lungu na kumuingiza Chimwemwe Idana.

Mabadiliko hayo hayakuisaidia Bullets kwani dakika tano baadaye Simba ilipata bao la kwanza kupitia Phiri aliyewazidi akili mabeki wa Nyasa na kumtungua kipaClever Mkungula akitumia pasi safi ya Chama.

Kipa wa Bullets alifanya kazi nzuri dakika ya 42 kuzuia mpira uliokuwa ukienda wavuni uliopigwa na kiungo Sadio Kanoute na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 1-0.

Kipindi cha pili Bullets ilirejea na mabadiliko ikiwatoa Macphallen Ngwira na Antony Mfune na kuwaingiza Righteous Banda na Adepoju Baba Tunde.

Katika dakika ya 48 timu hiyo ilitengeneza shambulizi kali na mkwaju mkali wa Ernest Petro ukaokolewa na kipa Aishi Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 50, Simba ilipata bao la pili likitupiwa tena kambani na Phiri safari hii alibadilisha mguu tu kwani alifunga kwa shuti la mguu wa kushoto akimaliza pasi murua ya Okrah.

Bao hilo liliizamisha Bullets na kuongeza mashambulizi yaliyoishia kwa mabeki wa Simba .

Simba ilimtoa Kibu dakika ya 60 na kumuingiza Osmane Skaho kabla ya kumtoa Phiri na kumuingiza Dejan Georgijevic kisha Chama na Okrah walitoka kuwapisha Peter Banda na Nelson Okwa.

Dakika ya 86 Simba ilitengeneza nafasi nzuri kupata bao la tatu pasi ya kisigino ya Dejan, ilishindwa kumalizwa wavuni na Sakho.

Matokeo hayo yameifanya Simba kuungana na Yanga kutinga raundi ya kwanza, sambamba na Kipanga ya Zanzibar zilizofuzu juzi kwa kuzitoa Zalan na Al Hilal Wau zote za Sudan Kusini.

Kocha Mgunda alisema anashukuru kwa kuvuka salama, huku akiwapongeza wachezaji kwa walivyocheza akikiri Bullets haikuwa timu nyepesi licha ya kuwang’oa.

Phiri kwa upande wake aliwapongeza wachezaji wenzake kwa kupambana hadi kuvuka na kumisifia Chama kwa kumtengenezea bao jingine kama alivyofanya mjini Lilongwe na kumfanya afikishe mabao matatu katika michuano hiyo.

Vikosi vilivyocheza;

SIMBA- Manula, Mwenda, Tshabalala, Inonga/Ouattara, Kennedy, Kanoute, Mzamiru, Kibu/Sakho, Chama/Okwa, Okrah/Banda, Phiri/Dejan.

NYASA-Mkungula, Lanjesi, Sambani, Kajoke, Petro, Lungu/Chimwemwe, Chirwa, Kabichi/Mpokela, Willard, Phiri, Mfune/Banda, Ngwira/BabaTunde

Mechi zijazo za raundi ya kwanza zionatarajiwa kupigwa kati ya Oktoba 7-16 ambapo Simba itacheza na mshindi kati ya Red Arrows ya Zambia au Premiero do Agosto ya Angola, huku Yanga itaumana na mshindi kati ya Al Hilal ya Sudan au St George zilizopepetana usiku wa jana na kwenye Kombe la Shirikisho Kipanga ya Zanzibar itavaana na Claub African ya Tunisia.


KAGERA v DODOMA

Wakati huo huo katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa jana mjini Bukoba, wenyeji Kagera Sugar walilazimishwa suluhu na Dodoma Jiji. Mechi hiyo ilipigwa Uwanja wa Kaitaba na kuzifanya timu hizo kugawana pointi na kila moja kufikisha pointi mbili baada ya mechi nne.

Leo ligi hiyo itaendelea kwa kiporo cha Ruvu Shooting dhidi ya Polisi Tanzania.