Prime
Oura, Simba... Ngoma ngumu ishu ipo hivi!
KLABU tatu kutoka Barani Ulaya zimeripotiwa kuanza harakati za kupata huduma ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Anicet Oura ambaye alifanikiwa kuonyesha kiwango cha juu kwenye msimu uliomalizika.
Kiungo huyo raia wa Ivory Coast amefanikiwa kuonyesha kiwango cha juu akiwa na kikosi cha Simba ambacho alikitumikia kuanzia Januari mwaka huu hadi mwishoni mwa msimu.
Mwanaspoti limebaini kuwa klabu zinazofuatilia kwa karibu Oura ni Bursaspor ya Uturuki, Víkingur Reykjavík ya Iceland na DAC 1904 Dunajská Streda ya Slovakia ambazo zimeanza kufanya tathmini ya uwezekano wa kumnasa mchezaji huyo.
Oura mwenye miaka 26, alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu akitokea IF Gnistan ya Finland kwa mkataba wa miaka miwili na tangu kutua Msimbazi amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika mafanikio ya timu hiyo msimu huu.
Kiungo huyo mshambuliaji alisaidia Simba kutwaa mataji mawili ya Kombe la CRDB na Muungano huku akionyesha uwezo mkubwa katika eneo la kiungo mshambuliaji kwa kufunga mabao sita na kutoa asisti tatu kwenye ligi ambako wekundu hao walimaliza wakiwa nafasi ya pili na pointi 73, nyuma ya Yanga ambayo ilitwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi mbili.
Uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti kwenye safu ya ushambuliaji, kasi, nguvu na uwezo wa kutengeneza nafasi, umeifanya thamani yake kuanza kupanda kwenye soko la usajili.
Kabla ya kujiunga na Simba, Oura amepitia klabu mbalimbali zikiwemo Gnistan ya Finland, Muaither SC ya Qatar, Stellenbosch FC ya Afrika Kusini na ASEC Mimosas ya Ivory Coast kote akitajwa kama mmoja kati ya wachezaji mahiri.
MKWANJA MEZANI
Bursaspor ya Uturuki inaonekana kuongoza vita ya kumnasa Oura huku ikiwa tayari kuwasilisha ofa ya Euro 250,000 ambazo ni zaidi ya Sh 750 milioni.
Klabu hiyo si ngeni kwa Oura, kwani ilikuwa imeanza kumfuatilia tangu kipindi ambacho kiungo huyo mshambuliaji alipokuwa akicheza soka la kulipwa Finland kabla ya kukumbwa na majeraha.
Akizungumzia dili hilo, Wakala wa staa huyo, Serkan Dag alisema; "Oura amekuwa na msimu mzuri na ni kawaida kwa wachezaji wanaofanya vizuri kupata ofa mpya. Tutazungumza na Simba na kuona jambo ambalo litakuwa bora kwa pande zote mbili kwa sababu hata wakati mteja wangu akitua Simba tulikuwa na makubaliano na anaamini tulifanya uchanguzi sahihi."
BARKER AGOMEA
Kocha wa Simba, Steve Barker ameonyesha wazi kuwa Oura ni sehemu ya mipango yake kuelekea msimu ujao, akiamini bado ana uwezo mkubwa wa kuisaidia timu hiyo baada ya kuzoea soka la Tanzania.
"Ni mmoja wa wachezaji ambao ningependa kuendelea kuwa nao msimu ujao. Ana ubora, ana nidhamu na ana uwezo wa kusaidia timu yetu kufikia malengo makubwa," alisema Barker.
Kwa sasa Simba haijaweka wazi msimamo wake kuhusu hatma ya Oura, lakini uwepo wa klabu hizo tatu unaonyesha namna thamani ya mchezaji huyo imepanda ndani ya miezi michache tangu kuwasili Tanzania huku akiwa na mkataba bado wa mwaka mmoja na nusu.