Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SI MCHEZO: Saa moja ndani ya klabu ya Corinthians

Kuna duka kubwa kwa ajili ya bidhaa zao tu. Kila kitu unachonunua humo ni asilia. Hakuna kitu feki. Kuna kila kitu, jezi zao, fulana zao za aina mbalimbali, viatu, mataulo, mifuko, vifaa vya watoto, vikombe vya kunywea chai, miamvuli na vitu vingine kibao. Kila kitu kimeandikwa Corinthians.

Muktasari:

  • Eneo la klabu ya Corinthians ni mara tatu ya eneo la Chamazi ambapo klabu ya Azam imejitutumua kwa kiasi kikubwa kujenga uwanja wa kisasa maeneo ya Mbagala.

KATIKA Mtaa wa Sao Jorge, nje kidogo ya Jiji la Sao Paulo hapa Brazil ndipo yalipo makazi ya klabu ya Ligi Kuu Brazil, Corinthians. Ni ndoto ya mchana kuwepo eneo hilo. Pindi unapokuwapo unagundua wengine tunapoteza muda tu katika mchezo wa soka.

Hapa ndipo walipopita akina Paulinho, Javier Mascherano, Carlos Tevez, mkali wa soka wa Brazil katika kikosi cha mwaka 1970, Revelino, Vampeta na wengineo wengi. Ronaldo de Lima alipita mwaka 2009 wakati alipochoka soka la Ulaya.

Ni katika makazi ya Corinthians ndipo unapogundua kuwa watu wapo bize na maisha ya soka. Ndipo unapogundua kuwa soka ni maisha ya watu. Ndipo unapogundua kuwa klabu zetu zinafanya mzaha na mchezo wa soka.

Eneo la klabu ya Corinthians ni mara tatu ya eneo la Chamazi ambapo klabu ya Azam imejitutumua kwa kiasi kikubwa kujenga uwanja wa kisasa maeneo ya Mbagala. Kumbuka Azam ndio klabu pekee Afrika Mashariki yenye uwanja wake unaokubalika hata kwa mechi za kimataifa za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Lakini kwa Corinthians, soka sio mchezo pekee unaopatikana pale.

Kuna viwanja vitano vya kisasa vya mchezo wa tenisi, kuna mabwawa zaidi ya manne ya kuogolea. Kuna viwanja viwili kwa ajili ya mpira wa kwenye sakafu (Futsball), kuna viwanja viwili vya kisasa vya mchezo wa kikapu.

Kuna viwanja zaidi ya vinne kwa ajili ya timu za vijana chini ya umri wa miaka 19, 17, 16, 10. Watoto wenye umri wa chini ya miaka minane wanapelekwa na wazazi wao mwishoni mwa wiki.

Kutokana na mazoezi ya timu ya wakubwa kuhitaji faragha, timu hiyo haifanyi mazoezi hapo. Inafanya mazoezi katika viwanja vingine vilivyopo mwendo wa dakika 20 kutoka hapo. Huko ndipo akina Alexander Pato wanafanya mazoezi, lakini kwa sababu ya fainali za Kombe la Dunia, mazoezi yamesimama.

Achilia viwanja, ndani ya eneo hilo hilo, kuna jumba kubwa la makumbusho ya klabu hiyo. Ndani yake kuna historia nene ya klabu hiyo. Hawajasahau kitu. Kuna makombe yao yote ya zamani na sasa tangu klabu ilipoanzishwa mwaka 1910.

Kuna jezi zilizovaliwa na akina Revelino, Ronaldo de Lima, Tevez na wengineo. Kuna mipira iliyosainiwa. Kuna picha. Kuna televisheni mbalimbali zinazoonyesha mechi za fainali walizotwaa mataji makubwa na madogo.

Wamewahi kutwaa ubingwa wa kwao mara kadhaa. Wametwaa Klabu Bingwa ya Dunia, wametwaa Klabu Bingwa Amerika Kusini, wametwaa mataji mengi na kuna kila ushahidi.

Kuna sehemu ambayo wachezaji wao maarufu wa zamani wamekanyaga na kuacha nyayo zao. Unaziona wazi nyayo za Revelino na Ze Maria. Unapata hisia kali na kujua kuwa wenzetu wanaelewa maana ya soka.

Baada ya hapo kuna duka kubwa kwa ajili ya bidhaa zao tu. Kila kitu unachonunua humo ni asilia. Hakuna kitu feki. Kuna kila kitu, jezi zao, fulana zao za aina mbalimbali, viatu, mataulo, mifuko, vifaa vya watoto, vikombe vya kunywea chai, miamvuli na vitu vingine kibao. Kila kitu kimeandikwa Corinthians.

Hadi kufikia hapo haupati shaka kujua ni kwa nini walifanikiwa kumrudisha Ronaldo de Lima kutoka AC Milan na kuweza kumlipa mshahara wake mkubwa.

Ndani ya eneo la Corinthians kila mtu yuko bize. Dukani kuna wafanyakazi kama wanane. Lakini kama ukijumlisha idadi ya kila idara ndani ya eneo hili, kunaweza kuwa na wafanyakazi 200 hivi. Ni eneo ambalo hauwezi kuamini kuwa makao makuu ya klabu ya soka.

Macho yangu yanavutiwa zaidi na mazoezi ya timu ya vijana. Wote wanaonekana kuwa makini na mazoezi kabla hata hayajaanza. Wanavaa viatu kwa ukimya. Wanaongea kwa adabu. Kila mtu anaonekana anatembea na ndoto yake.

“Nataka kucheza Ulaya. Nataka kucheza Real Madrid na naamini nitafanikiwa haraka iwezekanavyo. Mchezaji anayenivutia na ambaye nataka kucheza kama yeye ni Neymar,” anasema Ricardo Aruajo, kinda mwenye umri wa miaka 15 ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji katika kikosi cha Corinthians chini ya umri wa miaka 16.

Kinda mwingine ambaye nazungumza naye ni Ricardo Pereira ambaye anavutiwa zaidi na uchezaji wa beki wa Chelsea anayehamia PSG, David Luiz.

“Nacheza beki. Ndoto yangu ni kuichezea timu ya taifa katika michuano ya Dunia kama hii. Napenda sana uchezaji wa David Luiz na siku moja nitakuwa kama yeye,” anasema Pereira huku akivaa viatu vyake na kutokomea katika uwanja wa mazoezi.

Makinda wengine wawili, Thiago Gomes na Jarmes Juveio wanaonekana kuhamasika zaidi na wachezaji wenye majina makubwa. Thiago ambaye anataka kufikia mafanikio ya Oscar anazungumza jinsi wachezaji wa timu kubwa wanavyokuja kuwatia hamasa.

“Wachezaji wa timu kubwa huwa wanafika hapa kututia hamasa sana. Wao ndio vioo vyetu. Wengi wametoka katika timu hizi za vijana ambazo na sisi tunapitia kwa hiyo wanakuja kututia moyo,” anasema Thiago ambaye ana umri wa miaka 14 tu.

Kikubwa kinachoonekana ni kwamba makinda hawa wana nidhamu ya hali ya juu. Hawabwatuki ovyo. Hawafanyi mambo ovyoovyo. Wazazi wao wanalipa kwa ajili ya wao kutafuta maisha ya soka. Wakionyesha viwango vya hali ya juu ndipo klabu inaingia nao mikataba ya kulipwa au inaanza kuwalipia shuleni.

Wengi wameniahidi kwamba sitachukua muda mrefu kabla sijawaona katika klabu za Real Madrid, Barcelona, Corinthians ya wakubwa, AC Milan na nyingine. Ukiwatazama walivyo makini, hakuna unachoweza kuwabishia.

Endelea kutembelea tovuti ya Mwanaspoti, wiki hii nitatembelea klabu ya Santos ambayo iliwakuza Pele, Neymar na Robinho.