Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shoo kama kawa, Kwa Mkapa anaumia mtu

Wahezaji wa Yanga, Fiston Mayele akishangilia bao lake baada kupokea pasi kutoka kwa Saido Ntibazonkiza.

TUNAANZIA tulipoishia. Ndivyo wanavyosema mashabiki wa Yanga wakati chama lao leo usiku likitarajiwa kushuka tena uwanjani kuvaana na Kagera Sugar katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Baada ya kumaliza kibabe duru la kwanza la ligi hiyo, Yanga leo inashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya kwanza ya duru la pili dhidi ya Kagera, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Mchezo huo wa leo ni kati ya mechi 11 ambazo Yanga itacheza ndani ya jijini Dar es salaam katika duru la pili, huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Kagera ugenini walipoifumua bao 1-0.

Ushindi wa nyumbani leo, utaifanya Yanga ifikishe pointi 42 na kutanua pengo la pointi baina yake na Simba iliyopo nafasi ya pili hadi kufikia 11, japo watani wao watakuwa na faida ya kuwa na mechi moja mkononi.

Kagera yenyewe kama itaibuka na ushindi itafikisha pointi 23 na kusogea hadi nafasi ya tano katika msimamo.

Licha ya kuwakosa baadhi ya nyota katika mchezo wa leo kutokana na majeraha na wengine kutumikia adhabu, kocha Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi bado wana wachezaji wazuri wanaoweza kuipatia matokeo mazuri.

Yanga itaendelea kuwategemea zaidi Saido Ntibazonkiza na Fiston Mayele ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali katika kufumania nyavu na hata kupika mabao wakati Kagera yenyewe ikielekeza matumaini yake kwa Hassan Mwaterema, Erick Mwijage na Hamis Kiiza waliounda utatu unaoibeba timu hiyo kwa hivi karibuni.

Zinakutana timu mbili ambazo zimekuwa na mwendelezo bora wa matokeo Yanga ikiwa kinara kwa kutopoteza mechi yoyote ya ligi msimu huu hadi sasa ambapo imecheza jumla ya michezo 15, imeshinda 12 na kutoka sare katika mechi tatu. Rekodi zinaonyesha Yanga haijapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu tangu ilipofungwa mara ya mwisho ya Azam FC ka bao 1-0 kwenye mechi ya msimu uliopita iliyopigwa Aprili 25, 2021 na kuifanya hadi sasa ifikishe mechi 22 bila kuonja machungu ya vipigo.

Kwa upande wa Kagera tangu ilipofungwa bao 1-0 nyumbani na Prisons, Desemba 26, 2021, haijapoteza mechi tena katika mechi tano zilizofuata, ikiibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare mbili.

Yanga imekuwa na historia ya kufanya vizuri kila inapokutana na Kagera katika Ligi Kuu na matokeo ya mechi 10 zilizopita baina yao ni uthibitisho tosha wa hilo.

Katika mechi hizo, Yanga imeshinda mara nane, Kagera ikishinda mara moja na pia zimetoka sare katika mechi moja.

Makocha wa pande zote, wametambiana kuwa timu zao zipo tayari kuonyesha shoo ya maana na kusaka ushindi ili kujiweka pazuri kwenye msimamo, licha ya kila mmoja kukiri kwamba wapinzani wao ni wazuri.

Francis Baraza alisema anaiheshimu Yanga, lakini bado anahitaji ushindi katika mchezo huo, huku Nabi akisisitiza hataki kudondosha pointi katika mechi ya nyumbani baada ya mechi yao iliyopita dhidi ya Mbeya City kutoka suluhu.

Kabla ya mechi hiyo ya usiku jijini Dar, mapema saa 10 jioni ya leo kutakuwa na pambano jingine tamu la Ruvu Shooting itakayoikaribisha Dodoma Jiji, mechi itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, ambapo ushindi utawasogeza wenyeji hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi.

Mchezo mwingine utapigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kwa wenyeji Tanzania Prisons inayoshika mkia itakapoumana na wapinzani wao wa jiji hilo, Mbeya City.