Serengeti Boys yaahidi furaha kwa Watanzania kesho

Muktasari:
Ushindi dhidi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Uganda, utafufua matumaini ya Serengeti Boys kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Brazil baadaye mwaka huu.
Dar es Salaam. Si kazi rahisi kwa wachezaji wa mpira wa miguu kupoteza haraka kumbukumbu za matokeo mabaya ambayo timu yao hupata kwenye mchezo fulani hasa wanapopoteza kwa idadi kubwa ya mabao tena wakicheza uwanja wa nyumbani.
Matokeo ya namna hiyo huweza kuwavuruga kisaikolojia na kuwafanya wawe kwenye presha kubwa inayopelekea timu nyingine kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata hasa ikiwa ya mfululizo inayochezwa ndani ta kipindi kifupi.
Hata hivyo hali iko tofauti kwa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' ambayo licha ya kupoteza mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa mashindano ya soka ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17), imetamba kutovurugwa na matokeo hayo na kutangaza hali ya hatari kwa wapinzani wao Uganda kwenye mchezo unaofuata.
Akizungumza muda mfupi baada ya mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya HOPAC jijini leo, Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo ametamba kuwa vijana wake wamefuta kumbukumbu mbaya iliyopita kwa haraka na wamejipanga kuiduwaza Uganda kwenye mchezo wa kesho.
"Kwanza tunafurahi na kushukuru kwamba vijana wako na mtazamo chanya kuelekea mchezo wa kesho. Ni kweli kwenye mchezo wa kwanza hatukupata matokeo kwa hiyo kivyovyote vile ni lazima unyongee kidogo
Lakini tumeshaweka nyuma kila kitu kwa sababu hatuwezi kuyageuza matokeo ya mchezo uliopita. Na kwa sasa hivi tunafanya mipango ya kuhakikisha tunatumia ipasavyo michezo miwili iliyobakia hasa mchezo wa kesho ambao ndio umeshikilia hatma
Kwa maana ya mazoezi na saikolojia ya vijana viko vizuri na tunaamini kwamba kesho tutakuwa na wakati mzuri ambao tunauhitaji sana kuliko mtu mwingine yeyote," alisema Mirambo.
Matokeo ya mchezo uliopita ambao Serengeti Boys ilipoteza mbele ya Nigeria, yameifanya ilazimike kusaka ushindi kwenye mechi mbili zijazo dhidi ya Uganda na Angola ili iweze kufuzu nusu fainali na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Brazil mwezi Oktoba.
Kwa sasa Serengeti Boys inashika mkia kwenye kundi A ikiwa haina pointi nyuma ya Nigeria inayoongoza, Angola iliyo nafasi ya pili na Uganda inayoshika nafasi ya tatu.