Serengeti Boys kukata utepe na Guinea Ulaya

Muktasari:
Mashindano hayo ambayo yatashirikisha mataifa 17, yameandaliwa na Shirikisho la Sola la Bara la Ulaya (Uefa) kwa lengo la kuzipa mazoezi na uzoefu timu mbali mbali kwa ajili ya mashindano tofauti.
Dar es Salaam. Timu ya soka ya Taifa ya chini ya miaka 17, Serengeti Boys imepangwa kufungua dimba Guinea katika mashindano maalum yaliyopangwa kufanyika mjini Antalya, Uturuki mwezi ujao.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopatikana jana, mbali ya kucheza na Guinea Machi 4, Serengeti Boys itacheza mchezo wake wa pili dhidi ya Australia Machi 6 na baadaye kucheza na wenyeji, Uturuki Machi 8.
Mashindano hayo ambayo yatashirikisha mataifa 17, yameandaliwa na Shirikisho la Sola la Bara la Ulaya (Uefa) kwa lengo la kuzipa mazoezi na uzoefu timu mbali mbali kwa ajili ya mashindano tofauti.
Serengeti Boys ambayo ipo katika kundi A la fainali za Afcon ambayo yatafanyika nchini, itapata bahati ya kucheza na Guinea ambayo ipo Kundi B. Timu nyingine ambazo zipo kundi A ni Nigeria na Uganda ambazo zimepangwa kundi moja pamoja na Morocco mjini Antalya.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ammy Ninje amesema kuwa jumla ya wachezaji 30 wa Serengeti Boys wapo kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa na mashindano hayo.
Ninje alisema kuwa wachezaji hao wataungana na wengine na kutengeneza timu mbili na kuweka kambi mkoani Arusha kwa maandalizi zaidi. Alisema kuwa wachezaji hao watapimwa kipimo cha kujua umri sahihi (MRI Test) na wataopita katika mchujo huo watachaguliwa kwa ajili ya kambi ya muda mrefu pamoja na kwenda Uturuki.
“Tuna wachezaji wengi wenye vipaji na wanatakiwa kuchezea nchi yao kwa ajili ya michuano ya Afcon kwa vijana yaliyopangwa kuanza April 14 mpaka 28 jijini. Kwa sasa wachezaji 30 wapo chini ya kocha mkuu, Oscar Mirambo wakijiandaa, lakini lazima tuchukue tahadhari ya umri kabla ya kutangaza kikosi kamili, hivyo, kipimo cha MRI ni cha lazima kufanyika kwa wachezaji wetu,” alisema Ninje.
Kuhusiana na mashindano ya Uturuki, Ninje alisema kuwa mipango inafanyika ili kuiwezesha timu yao kucheza na Nigeria na Cameroon ii kupata kipimo sahihi. Alisema kuw wanajua kuwa Nigeria inaweza kukataa kucheza kwa kuwa wapo kundi moja, lakini wanatarajia kupata mechi zaidi hata kama itashindikana kucheza na magwiji hao wa soka Barani Afrika.
Serengeti Boys itaanza kampeni za kutwaa ubingwa wa Afrika kwa vijana kwa kupambana na Nigeria Aprili 14 ba mechi ya pili itakuwa dhidi ya Angola Aprili 17 na kumaliza dhidi ya Uganda.
Kundi B lina timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal. Timu nne zitafuzu kucheza mashindano ya Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini Peru kuanzia Oktoba 5 mpaka 27 katika miji ya Lima, Piura, Tacna na Trujillo.