Sebo kukaa nje ya uwanja miezi mitatu

Uongozi wa Azam FC umetangaza beki Abdallah Kheri 'Sebo', atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti la mguu wa kulia.

Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imesema Sebo ameumiza gegedu 'cartilage' ya maungio ya goti lake la mguu wa kulia, ambayo imelika na pia ameumiza mifupa midogo midogo kutokana na mlalo wa goti lake la kulia na tege alilokuwa nalo.

Beki huyo kisiki, amefanyiwa upasuaji huo leo Jumatatu asubuhi, kwenye Hospitali ya Vincent Palloti, jijini Cape Town, Afrika Kusini.

Sebo alipata majeraha hayo kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya dhidi ya Tanzania Prisons, walioshinda mabao 3-1, ambapo alilazimika kutolewa wakati wa mapumziko, nafasi yake ikichukuliwa na Nathan Chilambo.

Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, aliyeambatana na beki huyo, amesema kuwa Sebo atarejea kwenye soka la ushindani baada ya miezi mitatu ya matibabu ya majeraha yake kumalizika.

"Sebo amefanyiwa upasuaji wa kisasa unaoitwa arthroscopic, ambao wametoa mifupa midogo midogo iliyokuwa imevunjika na kupandikiza gegedu nyingine.

"Baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mchezaji ameelekezwa mazoezi ya kufanya kwa muda wa mwezi mzima na anatakiwa kupumzika kwa muda wa miezi mitatu," amesema Dr. Mwankemwa.