Sauti Sisters yazidi kulizamisha jahazi la Warriors Queens

Muktasari:
- Nafasi ya nne ambayo ni ya mwisho, inashikiliwa na Warriors ambayo haina alama kutokana na kupoteza michezo yote mitatu.
KIPIGO cha mabao 2-1 ilichopokea Warriors Queens kutoka kwa Sauti Sisters, kimeifanya timu hiyo kuwa na hali mbaya zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Soka Wanawake Zanzibar.
Mchezo huo uliopigwa Juni 25, 2025 kwenye Uwanja Mao B, Unguja, umehitimisha mzunguko wa tatu wa ligi hiyo, ambapo Warriors bado haijaonja ladha ya ushindi ikipoteza michezo yote mitatu na kuburuza mkia katika msimamo.
Warriors haikupoteza kwa bahati mbaya kwani katika mchezo huo, Sauti Sisters ilipoteza nafasi saba za wazi na kutumia vizuri mbili zilizozaa mabao hayo.
Licha ya Sauti kuibuka na ushindi huo na kuonekana kushambulia zaidi katika lango la wapinzani wao, lakini bado haikuwa na muunganiko mzuri eneo la mwisho la ushambuliaji iliyowafanya kupoteza mipira mara kwa mara.
Katika kukamilisha mzunguko wa tatu wa ligi hiyo, JKU Princess inaongoza msimamo kwa kuwa na alama saba, ikishinda michezo miwili na sare mmoja, ikifunga mabao 11 na kuruhusu moja.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Dunga Queens iliyoshinda michezo miwili na kupoteza mmoja ikivuna alama sita. Pia imefunga mabao sita na nyavu zao kutikiswa mara 12, ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi katika ligi hiyo.
Sauti Sisters ipo nafasi ya tatu kwa kushinda mchezo mmoja kati ya mitatu huku ikipoteza mmoja sawa na sare, ikivuna alama nne. Imefunga mabao manne na kufungwa matano.
Nafasi ya nne ambayo ni ya mwisho, inashikiliwa na Warriors ambayo haina alama kutokana na kupoteza michezo yote mitatu. Imefunga mabao matatu na kuruhusu sita.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea Jumapili Juni 29, 2025 kwenye Uwanja wa Mao B ambapo Dunga Queens itaikaribisha JKU Princess.