Samatta asifia mbinu za Kim

MASAA machache yamebaki kuelekea mechi ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Africa (Afcon) kati ya Guinea ya Ikweta mchezo unaotarajiwa kupigwa Alhamisi ya leo saa 4:00 kwenye dimba la Nuevo Estadio de Malabo.

Mchezo huo ambao Stars watahitaji ushindi au sare ili kufufua matumaini ya kuendelea kusonga mbele na endapo watapoteza mechi hiyo basi rasmi watakua wamejiondosha katika mbio za kushiriki Afcon inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Cameroon.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta amesema wanatambua umuhimu wa mechi hiyo na wanaamini katika mbinu na uwezo wa kocha mkuu wa kikosi hicho Kim Poulsen katika kuwapa ushindi leo.

“Nimefanya kazi na Kim tangu akiwa timu ya taifa na vijana, ni kocha ambaye yuko vizuri wakati wote pia mifumo yake naifahamu na inaweza kutusaidia, tunafahamu kwamba mchezo huu ni kama fainali kwetu, hatutaenda kupambana kizembe bali kutafuta matokeo,” amesema Samatta.

Pia kocha Kim ameelezea maandalizi ya timu kwa ujumla na kuahidi ushindi kwenye mechi hiyo.

“Tumejiandaa vizuri na ni ndoto ya kila mchezaji kufuzu na kushiriki Afcon, tulicheza na Guinea ya Ikweta ambao nao wanahitaji ushindi kama ilivyo kwetu hivyo tunaenda kupambana ili tupate ushindi,” amesema Kim.

Endapo Stars watashinda mchezo huo watakuwa wamebakiza alama tatu tu kufuzu Afcon mwakani ambapo bado wanamchezo wa marudiano na Libya Machi 28 mechi ambayo wakishinda watakuwa wamefuzu kucheza Afcon Mwakani.

Katika kundi J ilipo Stars kuna jumla ya timu nne za Tunisia ambao tayari wamekwisha fuzu  wakiwa na alama 10, Guinea ya Ikweta yenye alama sita na Libya ambayo imefungana na Stars wote wakiwa wamevuna alama nne hivyo kwa hesabu za haraka Stars inahitaji kushinda michezo yote miwili iliyobaki.