Safu ya ushambuliaji Yanga balaa

YANGA imekamilisha usajili wa safu yao ya ushambuliaji baada ya kumleta nchini straika wao wa zamani Heritier Makambo ‘Mzee wa Kuwajaza’.

Makambo aliyejipatia umaarufu kufuatia staili yake ya kushangilia ametua jana usiku kisha kupokewa na kigogo wa Yanga, Godson Karigo.

Ujio wa Makambo ni kwamba sasa Yanga imekamilisha kuunda safu yao mpya ya mshambuliaji itakayokuwa na Wakongomani wawili pale kati akicheza sambamba na Fiston Mayele.

Mayele mapema juzi usiku alisaini mkataba wa miaka miwili kuanza kuitumikia Yanga huku wenyewe wakimtambulisha rasmi akipewa jezi namba 9.

Mayele alikuwa jukwaani uwanjani kwa Mkapa jana sambamba na Mkongomani mwenzake Mukoko Tonombe kisha akawasalimia mashabiki wa timu hiyo wakati Yanga ikicheza mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Kagame dhidi ya Big Bullets ya Malawi.

Mara baada ya kutua Makambo ambaye aliifungia Yanga mabao 17 msimu wa 2017-2018 kabla ya kuuzwa Horoya ya Guinea hakutaka kuongea kitu baada ya kuzuiwa na uongozi wa Yanga.