Sababu ya Mabula kurejeshwa Taifa Stars

Muktasari:
- Jana kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ameita kikosi cha wachezaji 28 kitakachoingia kambini Juni 2 kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) na mashindano ya COSAFA dhidi ya Eswatini na Madagascar.
MWEZI uliopita Mwanaspoti iliandika uchambuzi namna kiungo Alphonce Mabula anavyoitaka namba kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ baada ya kukosekana kwa takribani miaka minne.
Jana kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ameita kikosi cha wachezaji 28 kitakachoingia kambini Juni 2 kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) na mashindano ya COSAFA dhidi ya Eswatini na Madagascar.
Kati ya nyota hao 28 Mabula alikuwa miongoni mwao akirejea baada ya mara ya mwisho kuitwa katika kikosi hicho ilikuwa Februari 22, 2021 kwenye mashindano ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U-20 dhidi ya Morocco akikaa benchini.
Sababu kubwa ya kuitwa nyota huyo ni pamoja na kiwango bora alichoonyesha msimu huu akiwa na Shamakhi FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Azerbaijan.
Katika mechi 17 alizocheza Mabula alifunga mabao matatu akisaidia chama hilo kumaliza nafasi ya saba kati ya 10 zinazoshiriki ligi hiyo.
Akizungumzia baada ya kuitwa Stars Mabula alisema; “Ni ndoto ya kila mchezaji kuichezea timu yake ya taifa, nashukuru kwa kuitwa na naamini ndoto yangu imetimia maana nimechezea timu za vijana tu,”
Chama hilo limemaliza nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kwenye mechi 36 likishinda mechi tisa, sare tisa na kupoteza mechi 18 likikusanya pointi 36.
Ubora wake umemfanya hivi karibuni kuongezewa mkataba wa mwaka mmoja baada ya ule wa awali wa miezi 6 kukaribia ukingoni.
“Ofa ilikuwa nzuri ndio maana nimeongeza mkataba wa mwaka mmoja lakini pia nimefanya vizuri kwenye mechi chache na klabu iliniamini ikaniongezea mkataba kwa sababu ule wa awali ulikuwa wa miezi sita wenye kipengele cha kuongezewa.”