Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saa 72 za mtego Simba

SIMBA Pict

Muktasari:

  • Baada ya Simba kukosa taji hilo, kwa sasa Simba inakabiliwa na siku tatu ngumu sawa na saa 72 za kujua hatima yake msimu huu, huku kikosi cha Singida Black Stars kikishikilia hilo na kazi inaanza Jumatano hii.

DAKIKA 90 zilizopita zilikuwa na maumivu makali kwa Simba baada ya kushuhudia ikipoteza nafasi ya kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya RS Berkane kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Sare hiyo iliifanya Simba kupoteza fainali kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya ugenini kufungwa 2-0.

Baada ya Simba kukosa taji hilo, kwa sasa Simba inakabiliwa na siku tatu ngumu sawa na saa 72 za kujua hatima yake msimu huu, huku kikosi cha Singida Black Stars kikishikilia hilo na kazi inaanza Jumatano hii.

Kitendo cha kukosa ubingwa huo, kinaifanya Simba kuanza kupiga hesabu za mataji mawili yaliyobakia ambayo ni Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) yote yakishikiliwa na watani zao wa jadi, Yanga.

Katika Ligi Kuu Bara, Simba inashika nafasi ya pili ikivuna pointi 69 baada ya kucheza mechi 26, ipo nyuma ya vinara Yanga inayoongoza msimamo na pointi 73, lakini ina mechi moja zaidi, jambo linalozidi kuipa presha ya kuwania ubingwa huo pia.

Wakati timu hizo zote zikifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kujihakikishia kumaliza nafasi ya kwanza na ya pili, kazi iliyobakia ni ya ubingwa ambao Simba inauhitaji ili kurejesha matumaini ya mashabiki wa kikosi hicho.

Sasa wakati hilo likiendelea, Simba imebakisha mechi moja mkononi ili kutimiza 27, sawa na Yanga, itaanza kibarua hicho Jumatano hii kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam itakapoikaribisha Singida Black Stars.

Mechi hiyo ya kiporo, huenda ikatoa mwelekeo wa kikosi hicho katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kabla ya kukutana dhidi ya Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo, Juni 15, 2025, baada ya ile iliyopangwa, Machi 8, 2025, kuota mbawa.

Simba inakabiliwa na mechi hiyo dhidi ya Singida ambapo baada ya hapo, timu hizo zitakutana tena siku tatu zijazo katika nusu fainali ya Kombe la FA, Mei 31, 2025, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati, Manyara.

Mechi hizo mbili ni muhimu kwa Simba katika kuwania mataji yaliyobakia msimu huu, ambapo tayari Yanga iko kileleni mwa msimamo, huku pia ikiwa imeshatangulia fainali ya Kombe la FA, ikiifunga JKT Tanzania mabao 2-0.

Ndani ya siku hizo tatu, zinaweza kuamua hatima ya Simba msimu huu katika kuwania mataji mawili, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, ingawa kwa Singida Black Stars unaweza kusema haina cha kupoteza baada ya kujihakikishia nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu ujao.

Timu hiyo imepata tiketi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao baada ya Yanga kuifunga JKT Tanzania mabao 2-0, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA, hivyo kujihakikishia kumaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.

Iko hivi, bingwa wa Kombe la FA anapata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, ingawa kitendo cha Yanga na Simba kujihakikishia kumaliza nafasi ya kwanza na ya pili katika Ligi Kuu kimezipa nafasi Singida Black Stars na Azam FC kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho msimu ujao.

Kaimu Kocha Mkuu wa Singida, David Ouma, alisema; “Tunaenda kucheza mechi mbili mfululizo na Simba ambazo kwetu tunazichukua kwa umuhimu mkubwa sana, malengo yetu makubwa yalikuwa ni kupata tiketi ya CAF ambayo tayari tumefanikiwa, sasa kilichobakia ni kuendeleza heshima yetu tu. Ukiangalia mpinzani wetu ametoka kucheza fainali ya Shirikisho, hivyo itatupa mwanga mzuri wa tunapokwenda CAF.”

Singida iliyo nafasi ya nne na pointi zake 53, baada ya kucheza mechi 27, ikishinda 16, sare tano na kupoteza sita, inakabiliana na Simba huku ikikumbuka kichapo cha bao 1-0 ilichopata mara ya mwisho zilipokutana Desemba 28, 2024 kwenye Uwanja wa Liti, Singida kupitia bao la Fabrice Ngoma.

Wakati zinakutana katika mchezo wa duru la kwanza, Simba ilikuwa kileleni mwa msimamo na pointi 37, Singida Black Stars ya nne ikikusanya pointi 33 tofauti ikiwa nne. Lakini sasa Simba ni ya pili na pointi 69, Singida ya nne pointi 53. Tofauti pointi 13.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alisema: “Itakuwa mechi nzuri na ushindani mkubwa sana, ya kwanza tulishinda 1-0, licha ya ugumu wao tutahakikisha tunashinda. Ratiba imekuwa ngumu, tulikuwa tunalitambua hilo na tumejiandaa kukabiliana nalo.”

Matola alibainisha kwamba, mchezo dhidi ya Singida Black Stars watacheza kwa mbinu tofauti na ilivyokuwa fainali dhidi ay RS Berkane huku akitaja sababu kubwa ni kwamba michuano hiyo ni tofauti.

“Kila mechi ina mbinu zake, fainali ya CAF ishaisha, mechi ya kesho (leo) itakuwa na mbinu tofauti kwani sio sawa na ilivyokuwa fainali kwani ni michuano tofauti.

“Wachezaji ni waelewa, baada ya fainali na kukosa ubingwa huku malengo yakiwa ni kushinda, saikolojia yao imevurugika, lakini tumefanya kikao na kuwaambia kwamba yale yameisha na malengo ni kuchukua ubingwa wa ndani na hatuwezi kuwa mabingwa bila ya kushinda, hivyo tunaanza kesho kuhakikisha tunakuwa mabingwa msimu huu,” alisema Matola.