Ruvu Shooting, KMC wajifua Sokoine kuzikabili City, Mbeya Kwanza

Mbeya. Timu za Ruvu Shooting na KMC zimefanya mazoezi kujiweka sawa na mechi zao za Ligi Kuu watakazocheza katika uwanja wa Sokoine jijini hapa.
Timu hizo za Pwani na Dar es Salaam zimegongana uwanja wa Sokoine Mbeya na kuamua kugawana eneo kwa ajili ya kujifua tayari kwa mechi zao za raundi ya 13 ya Ligi Kuu Bara.
Ruvu Shooting inajiandaa na mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kesho Alhamisi, huku KMC ikiwa inajiwinda na Mbeya Kwanza mpambano utakaofanyika Ijumaa, mechi zote zikipigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Maafande hao wakiwa chini ya Kocha wao Mkuu, Charles Mkwassa hawakutumia muda mrefu kujifua ambapo takribani saa 1 liliwatosha kumaliza kazi.
Mkwassa alionekana kuwapa matizi ya fiziki, pumzi na pasi fupifupi na baadaye kuhitimisha na kufunga mabao huku nyota wake wakionekana kuwa na mzuka sana.
Kwa upande wa KMC chini ya Kocha wao, Hitimana Thiery walitumia zaidi ya masaa matatu kupiga tizi ambapo walianza na kutafuta pumzi, kukaba, kupiga pasi na kuhitimisha kwa kufunga mabao ya vichwa.
Ikumbukwe KMC inawakabiri wapinzani hao, ambapo wenyeji wanakumbuka kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Azam bao 1-0, huku vijana hao wa Kinondoni wakishinda dhidi ya Tanzania Prisons mabao 2-0 ugenini.