Robertinho, Nabi washindwe wao tu

HAKUNA namna kwa makocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga kwenye mechi za raundi ya pili ya makundi ya michuano ya kimataifa barani Afrika.
Makocha hao walishuhudia timu hizo zikipoteza mechi za raundi ya kwanza zikiwa ugenini, Simba ikilala bao 1-0 mjini Conakry, Guinea katika Ligi ya Mabingwa ilipovaana na Horoya, ilihali Yanga ikiwa Tunis, Tunisia ilichapwa 2-0 na US Monastir kwenye Kombe la Shirikisho.
Wikiendi hii, timu hizo zinarudi nyumbani jijini Dar es Salaam kwa kuvikaribisha vigogo vya soka barani Afrika, Raja Casablanca ya Morocco na TP Mazembe kutoka DR Congo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba itaanza kutupa karata leo Jumamosi kwa kuikaribisha Raja kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa, kabla ya Yanga yenyewe kuwa wenyeji wa Mazembe kesho Jumapili mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho. Mechi zote zikitarajiwa kupigwa kuanzia saa 1:00 usiku.
Mechi hizo ni mtihani kwa makocha wote wawili, ambao wataziongoza kwa mara ya kwanza timu hizo kwenye mechi za makundi kwa msimu huu zikiwa nyumbani, lakini wakiwa na kibarua cha kuhakikisha wanasahihisha makosa ya mechi za kwanza kwa timu hizo kwa makundi hayo.
Hii itakuwa ni mechi ya kwanza kwa Simba na Raja kukutana kwenye mechi za kimataifa, lakini kwa Yanga hii ni mara ya pili kukutana na TP Mazembe katika michezo ya makundi ya Kombe la Shirikisho, kwani zilishakutana mara ya kwanza mwaka 2016 na Wakongo kushinda nje ndani.
MTIHANI MGUMU
Kazi kubwa itakuwa kwa Robertinho ambaye anaiongoza Simba kwa mara ya kwanza mbele ya Wamorocco wenye rekodi ya kubeba jumla ya mataji manane ya Afrika, yakiwamo matatu ya Ligi ya Mabingwa na mawili ya Shirikisho, mawili Super Cup na Kombe le Caf huku ikionekana kuwa tishio kwa miaka ya karibuni.
Maya ya mwisho Raja imebeba taji la CAF mwaka juzi tu, ilipobeba Kombe la Shirikisho na msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika ilifika robo fainali, kitu kinachoonyesha Kocha Robertinho ana kazi ya kufanya kwenye mechi mechi hiyo ya nyumbani.
Licha ya Simba kukutana mara ya kwanza na Raja, lakini ina kumbukumbu ya kucheza na timu kutoka Morocco mwaka 2011 kukutana na Wydad Casablanca, watetezi wa taji kwenye mechi maalum ya playoff ya Ligi ya Mabingwa baada ya Mazembe kuzingua na Simba kulala 3-0.
Hivyo, leo Simba itashuka uwanjani ikiwa na rekodi isiyovutia mbele ya Waromocco, lakini ikijivunia rekodi tamu ya uwanja wa nyumbani, kwani vigogo kadhaa vya Afrika vimepata aibu Kwa Mkapa kwa kucharazwa na Simba ikiwamo mabingwa wa kihistoria, Al Ahly.
Simba haijawahi kupoteza mechi ya makundi ikiwa nyumbani tangu iliporejea kwa kishindo katika michuano ya CAF miaka mitano iliyopita. Pia tangu ilipopoteza nyumbani kwenye mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika 2013 mbele ya Recreativo do Libolo ya Angola ilikaa miaka minane hadi kuja kupoteza tena kwenye mechi za aina hiyo kwa kufungwa na Jwaneg Galaxy ya Botswana na kutupwa michuano ya Kombe la Shirikisho na kukwamia hatua ya robo fainali.
Kwa upande wa Nabi anakumbana na timu yenye rekodi nzuri ya michuano ya CAF ikitwaa jumla ya mataji 11 ikiwamo matano ya Ligi ya Mabingwa na mawili ya Kombe la Shirikisho, huku ikishinda mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Real Bamako ya Mali kwa mabao 3-1.
Haitakuwa mechi nyepesi kwa Yanga, kutokana na rekodi za hivi karibuni za timu hiyo kwa mechi za nyumbani hasa za kimataifa, lakini kwa kulinganisha na matokeo ya mechi tano zilizopita kwa wageni wao, ni wazi vijana wa Nabi wakikomaa wanaweza kutoboa Kwa Mkapa.
Mazembe kwenye mechi tano zilizopita zikiwamo nne za Ligi Kuu na moja ya CAF, imeshinda mbili tu, moja ya Ligi Kuu ya DR Congo na nyingine ya michuano ya CAF katika kundi hilo la D, huku ikipoteza mbili na kutoka sare, zote zikiwa za ligi. Hii ni tofauti na Yanga ambayo katika mechi tano imeshinda nne mfululizo za Ligi Kuu na kupoteza moja ya Kombe la Shirikisho dhidi ya US Monastir, kitu inaonyesha kama mastaa wa Jangwani wataamua kukomaa na kuijua vyema Mazembe inaweza kufanya maajabu.
MAINGIZO MAPYA
Simba iliyowakosa baadhi ya nyota akiwamo Saido Ntibazonkiza, Peter Banda, Jonas Mkude, Augustine Okrah na Jimmyson Mwanuke kwenye mchezo wa ugenini, safari hii baadhi ya wachezaji hao watarejea kikosini baada ya kupona majeraha waliyokuwa nayo.
Saido ana nafasi kubwa ya kuanza kwenye mchezo wa kesho na tayari Kocha Robertinho alishaweka bayana anataka kumtumia kumaliza kazi akishirikiana na wenzake, huku Moses Phiri na Jean Baleke aliyewahi kukipiga Mazembe, wataachiwa msala eneo la ushambuliaji sambamba na Clatous Chama.
Kwa upande wa Yanga, huenda Nabi akaanza na Mudathir Yahya ambaye kwenye mechi ya ugenini alianzia benchi na kuingizwa kipindi cha pili, kama inavyotajiwa kwa Joyce Lomalisa na Kennedy Musonda walioingizwa kutoka benchi.
Musonda anaweza kuanza na Fiston Mayele eneo la ushambuliaji iwapo Nabi atabadili mfumo wa uchezaji kulinganisha na ule alioutumia ugenini ambao uliifanya timu ishindwe kutembea na kutofanya mashambulizi makali baada ya Mayele kuzuiwa kirahisi na Watunisia.
MTAJI MZURI
Simba na Yanga, zina faida kubwa kwenye mechi hizo za kwanza za nyumbani kutokana na kubebwa na mashabiki wao wanaotarajiwa kuujaza uwanjani kama njia ya kuwahamasisha wachezaji.
Klabu kama Al Ahly ya Misri na nyingine zilizowahi kukutana na Simba Kwa Mkapa zimewahi kukiri namna timu hiyo inavyobebwa na wingi wa mashabiki uwanjani ambao wanashangilia mwanzo mwisho, kitu ambacho Raja inatarajiwa kukutana nacho leo na TP Mazembe kesho dhidi ya Yanga.
Uwepo wa mashabiki hao wanaotajwa kama wachezaji wa 12 kwa timu za nyumbani, inaweza kuwapa nafuu wenyeji kupata ushindi utakaosaidia timu hizo kujiweka pazuri kwenye makundi yao kabla ya kusafiri kwenda ugenini tena kumaliza mechi za raundi ya tatu.
FAIDA ZAIDI
Makocha Robertinho na Nabi, watakuwa na faida nyingine ya ziada kutakata nyumbani ikitokana na ahadi tamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ametoa ahadi ya kununua kila bao la timu hizo kwenye mechi hizo za leo na kesho kwa Sh 5 milioni, kitu kinachoweza kuchochea mastaa wa Simba na Yanga kuigeukia kama fursa ya kuvunja fedha, lakini wakizibeba timu hizo kiulaini.
Ni wazi kina Mayele, Stephane Aziz KI, Phiri, Chama na Baleke watakuwa na kazi moja tu leo na kesho ya kuhakikisha wanatupia kambani kadiri wanavyoweza ili kuvuna fedha hizo kutoka kwa Rais Samia, lakini kuzirahisishia Simba na Yanga kwenye makundi yao.
Hata hivyo, ni wajibu wa mabeki wa timu zote sambamba na makipa wao, Aishi Manula na Diarra Djigui kuhakikisha hawaruhusu mabao langoni mwa timu hizo ili zipate ushindi.
Wachezaji kama hatari kama Patient Mwamba, Jephte Kitambala, Adam Bossu na wengine wa TP Mazembe ni wa kuchungwa na mabeki wa Yanga.
Kwa upande wa mabeki wa Simba wanapaswa kuwa makini na Zakaria Habti, Hamza Khabba, Yousri Bouzok na Jamal Harkass, beki anayejua kufunga.