Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RIPOTI MAALUMU: Ushirikina, ngono vyatesa wanasoka Bongo

Jana tuliona ushirikina unavyowasumbua baadhi ya wachezaji wakiamini katika mambo ya ndumba hususani wanapokumbana na majeraha. Pia tuliona vitendo vya ngono  vinavyowatesa miongoni mwao. Sasa endelea.....


MWENENDO WA MAISHA
Mwenendo na mitindo mibaya ya mchezaji muda mwingine husababisha ucheleweshwaji wa kupona kwa jeraha lake mfano ili jeraha liweze kuunga lazima kushikamana na ushauri wa daktari ikiwamo kupumzika, kutotumia kiungo hicho kabla ya muda ambao daktari amepanga.
"Mfano daktari akakuambia utapumzika kwa wiki mbili baada ya hapo ndio utaanza kukanyagia, sasa utakuta mchezaji anaanza kukanyaga kabla ya muda aliopangiwa, hivyo jeraha linakuwa limejitonesha na kuongezeka ukubwa.
"Hivyo ukifika ule muda aliopanga daktari kulingana na tatizo lililopo akitoa na muda wa ziada lakini utakuta mchezaji ni mlevi, hali chakula chenye virutubisho, hatulii nyumbani na muda huohuo unaona anakanyagia ule mguu kabla ya muda uliopangwa," anasema Dk. Shita.
Dk Yomba anasema wachezaji wengi hawafuati maelekezo ya tiba ndio maana hawaponi kwa muda sahihi na hata kama atapona jeraha litakuwa limejitengeneza kwa namna nyingine na hata kujirudia inakuwa rahisi.
Anasema siku moja akiwa timu ya taifa aligundua tatizo la mmoja wa wachezaji (jina tunalo) na wanatakiwa kwenda Uganda akafikisha taarifa kwa uongozi kwamba mchezaji huyo hawezi kucheza kutokana na tatizo lake.
Ikaleta utata sana kutokana na uwezo wake lakini nashukuru uongozi wa TFF ulinielewa na jina lake likakatwa japo kocha alilazimisha tuondoke naye.

"Jina lake lilipokatwa alinifuata akinilaumu lakini nikamwambia mpira ni kazi yako na mimi tiba ni kazi yangu sasa nikushauri kama utakubali nikushauri utacheza mpira kwa muda mrefu maana tatizo lako lilitakiwa ufanyiwe upasuaji
Yomba anasema mchezaji mwingine alikaa na tatizo lake tangu akiwa timu ya vijana akimshauri afanyiwe upasuaji lakini alikataa na mwisho wa siku baada ya miaka kadhaa akajikuta tatizo likiongezeka na kuishia kufanyiwa upasuaji na hadi sasa anauguza jeraha.


LISHE (SPORTS NUTRITION) MAJANGA 
"Mchezaji yeyote anayekuwa majeruhi anatakiwa kupangiwa mlo maalumu 'special diet' lakini katika hatua za awali kuna aina maalumu ya vyakula anatakiwa kula ili kujenga mwili na kusaidia uungaji wa jeraha mfano mbogamboga, maji ya kutosha na matunda.

Dk. Shita anasema hata baada ya kupona mchezaji anatakiwa kuwa kwenye uangalizi maalum wa chakula anachokula ili imsaidie sababu akiwa anakula vyakula kwa wingi bila mpangilio anaweza kujikuta ananenepena.
"Hapo ndio utaona umuhimu wa timu kuwa na wataalam wa lishe maana akinenepa kunakuwa na kazi ya ziada kumrejesha katika hali yake ya kawaida."
Dk Masunga anasema watu wa michezo huwa wana vyakula vyao maalum 'Sports Nutrition' ambacho mchezaji anapaswa kupewa kutokana na mazoezi anayofanya hivyo kitu kinachoingia ndani ya mwili kinatakiwa kiende kurudisha kile alichopoteza wakati wa mazoezi ili kumpa nguvu na kujenga mwili wake lakini wachezaji wengi hawawezi kwendana navyo kutokana na gharama.

"Tatizo wachezaji wengi wanapenda kula vyakula wanavyopenda wao sio kulingana na wataalam wanachoshauri kama vile mboga za majani. Utakuta mtu anakula chapati wakati labda ana majeraha na hafanyi mazoezi ya kutosha lakini timu chache zinazingatia lishe bora na kuwa na wataalamu wa kutoa semina kwa wachezaji hata kama akiwa nyumbani.
Anasema mchezaji aliyevunjika mfupa anatakiwa kupata chakula chenye madini ya 'kalsiamu' lakini wengine hutumia vidonge vyenye madini hayo.
Dk Mngazija anasema mchezaji anakula kulingana na tatizo alilonalo ili imsaidie kupona haraka mfano kwa mchezaji mwenye tatizo la kuchanika msuli anatakiwa kutumia chakula chenye vitamini C ambacho husaidia kamba za misuli kupona haraka.


UKOSEFU WA WATAALAMU
Dk Masunga anasema kuna wakati mchezaji anashindwa kurejea uwanjani kwa wakati sababu ni aina ya matibabu anayopewa mfano kwa mwenye tatizo la mishipa 'ligaments' kwa nchi kama zetu mchezaji anachukua muda mrefu sababu mazingira yetu na ukosefu wa wataalum wa kutosha.
"Mfano mchezaji anapotoka kwenye majeruhi anatakiwa kuwa na mtu maalum wa kumfanyia mazoezi na kupewa program yake na mtaalam maalum kwa ajili yake.

"Kwa ligi yetu kuna timu chache ambazo zina wataalamu hawa 'physical trainer' ndio maana baadhi ya timu mchezaji anapopata tatizo anarudi uwanjani hata kama hajapona vizuri sababu soka ndio ameweka maisha yake hapo.
Dk Mngazija anasema kushindwa kugundua tatizo sahihi kunasababisha wachezaji wengi kutopona kwa wakati sababu hata matibabu yanakuwa sio sahihi.

"Mfano mchezaji kaumia kichwani na damu inavujia ndani lakini ukaangalia nje pekee na kushughulika nalo ujue tatizo hilo halitapona kwa muda sahihi."
Anaongeza kama timu haina mtaalam wa lishe mara nyingi hutumia zaidi watu ambao wamesoma 'General medicine au Sports medicine' katika mambo mbalimbali.
Dk Yomba anasema sio tu kukosekana kwa wataalam wa lishe kwenye timu zetu bali hata suala la chakula ni changamoto na timu tatu ndizo zinazongatia hilo.

"Nilikuwa kwenye timu ya taifa kwa zaidi ya miaka sita, unachopendekeza ndicho wanachokitengeneza lakini tatizo la wataalam wa lishe hata kama akitafutwa na timu fulani hataweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo sababu sio jambo rahisi kwa timu kutekeleza.
Anasema ni gharama kubwa kwa kufuata mlo maalam kwa wachezaji ndio maana wachezaji wanaojitambua hutumia fedha zao binafsi sababu anajua mpira ni sehemu yake ya kazi na akifanya uzembe anaharibu maisha yake na hiyo inatokana na kupata somo la lishe.


WASIKIE WACHEZAJI
Emmanuel Gabriel 'Batgol' mchezaji wa zamani wa Simba, Tanzania Prisons na Friends Rangers anasema moja ya vitu vilivyomfanya kutundika daruga ni kutokana na jeraha la goti alilolipata.
"Niliumia nikiwa Uarabuni, lakini niliporejea nikiichezea Prisons msimu ulipoisha nikiwa mazoezini nyumbani nikakanyagwa, nikashindwa kuendelea na soka tatizo ambalo lilinisumbua kwa miaka miwili hivyo nikiwa Friends Rangers mwaka 2018 nikaachana kabisa na soka.
Allan Shomary nyota wa zamani wa Yanga anasema mwaka 1986 katika mchezo dhidi ya CDA ya Dodoma ambayo ilikuwa inasaka ushindi ibaki kwenye ligi lakini ikapoteza kwa mabao 2-0 na kwenye mchezo huo aliumizwa mguu baada ya kugongana na mchezaji wa CDA mfupa wa mguu ukaweka ufa.

"Nikapelekwa Muhimbili na kufungwa hogo nikaambiwa nipumzike kwa wiki kadhaa maana nilikua napata maumivu makali sana jambo lililokuwa likinifanya kushindwa hata kuuweka mguu chini."
Hata hivyo, Bakar Malima 'Jembe Ulaya' anasema kwake imekuwa bahati sababu hakuna jeraha kubwa alilopata na kumweka nje ya uwanja kwa muda mrefu kwani mwaka 1996 kwenye dabi aliumia goti lakini lilimweka nje wiki mbili tu.
"Tulipata bahati ya kuwa na mwalimu mzuri alikua anaitwa, Tambwe Leya ambaye siku zote alikuwa anasisitiza juu ya 'fitness' ya mchezaji ambapo tofauti na hapo majeraha yatakua yakikuandama kila wakati."

Anasema kipindi chao wachezaji walikua wanalipwa kupitia mapato ya mlangoni ndio maana mchezaji hata kama hajapona vizuri analazimisha kucheza huku uongozi nao kuna wakati unalazimisha hata kama daktari amekataza lakini kwa sasa ni uzembe wa mchezaji mwenyewe sababu hata asipocheza analipwa mshahara na mwisho wa siku madhara lazima yajitokeze.