Rasmi Dube kuikosa fainali FA dhidi ya Singida BS

Muktasari:
- Mapema leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi alisema bado hajawa na uhakika wa kumkosa mshambuliaji huyo, lakini sasa imethibitishwa rasmi kukosekana kwake.
YANGA imethibitisha rasmi kwamba katika mchezo wa fainali dhidi ya Singida Black Stars, mshambuliaji wao, Prince Dube hatakuwepo.
Mapema leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi alisema bado hajawa na uhakika wa kumkosa mshambuliaji huyo, lakini sasa imethibitishwa rasmi kukosekana kwake.
Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jioni ya leo kwenye Uwanja wa Aman, Dube hakuwa sehemu ya wachezaji waliofanya mazoezi hayo ambapo alionekana amekaa pembeni wenzake wakiendelea na pogram.
Dube ambaye hajapona vizuri majeraha ya nyama za paja, anaukosa mchezo huo utakaochezwa kesho Jumapili Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 2:15 usiku.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema: "Dube hatakuwepo katika mchezo wa kesho kwa sababu hali yake kiafya si nzuri.
"Hata mchezo uliopita (dhidi ya Simba) alicheza akiwa na majeraha, lakini ilibidi acheze kwani tulikaa na kukubaliana kwa pamoja aingie kufanya kazi maalum na kweli aliifanya."
Dube mwenye mabao mawili katika Kombe la FA msimu huu na 13 Ligi Kuu Bara, aliumia dakika ya 22 katika mchezo wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa Juni 18, 2025 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambapo Yanga ilishinda 5-0.
Majeraha hayo yalimfanya kuukosa mchezo uliofuata wa ligi Juni 22, 2025 dhidi ya Dodoma Jiji ulioipa Yanga ushindi mwingine wa 5-0, akaibukia Juni 25, 2025 dhidi ya Simba akianza kikosi cha kwanza na kumaliza dakika 45, akampisha Clement Mzize ambapo Yanga ilishinda 2-0 kupitia mabao ya Pacome Zouzoua na Mzize yote yakifungwa kipindi cha pili.