Rais Mwinyi aibeba Simba, alipia gharama zote Amaan

Muktasari:
- Hayo yameelezwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi Mawasiliano Ikulu, Zanzibar huku ikieleza uamuzi wa Rais Mwinyi unalenga kudhihirisha mapenzi yake ya dhati katika michezo pamoja na kuhamasisha ushindi kwa Simba, katika mechi hiyo ya kihistoria dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, ametoa zawadi maalum kwa timu ya Simba kwa kugharamia matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja utakaotumika kwa mechi ya fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho la Afrika, itakayofanyika Jumapili, Mei 25, 2025 kuanzia saa 10 jioni.
Hayo yameelezwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi Mawasiliano Ikulu, Zanzibar huku ikieleza uamuzi wa Rais Mwinyi unalenga kudhihirisha mapenzi yake ya dhati katika michezo pamoja na kuhamasisha ushindi kwa Simba, katika mechi hiyo ya kihistoria dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Imeongeza kuwa hatua hiyo pia ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuunga mkono maendeleo ya michezo na kuleta hadhi ya kimataifa.
Mbali na kuruhusu matumizi ya uwanja huo bure, Rais Mwinyi amechukua dhamana ya kugharamia maandalizi yote muhimu ya uwanja kwa mechi hiyo.
Aidha, fainali ya mechi hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa kutambua uzito wa mechi hiyo kwa taifa, Rais Mwinyi ameahidi kuhudhuria fainali hiyo sambamba na Watanzania wote katika kuwaunga mkono Simba na kuhamasisha ushindi wa kihistoria.
Simba imefika fainali ya michuano hiyo ya CAF kwa kuifunga Stellenbosch kwa bao 1-0 na katika mechi ya kwanza ya fainali ilipoteza ugenini mjini Berkane, Morocco kwa mabao 2-0 na Jumapili ina kibarua cha kushinda si chini ya mabao 3-0 ili kubeba taji kwa mara ya kwanza.