Rais Caf kufanya ziara ya siku moja Dar kesho

Muktasari:
- Ziara ya Motsepe katika mataifa matatu mwenyeji inaanza kesho Alhamisi asubuhi, Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam, Tanzania. Kisha atasafiri hadi Nairobi, Kenya na Kampala, Uganda siku ya Ijumaa, Desemba 20, 2024 ambapo atahitimisha ziara yake ya mataifa hayo matatu.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), Dokta. Patrice Motsepe, atazuru Tanzania, Kenya na Uganda - mataifa matatu ambayo yatakuwa mwenyeji wa Michuano ya Chan mwakani 2025.
Ziara ya Motsepe katika mataifa matatu mwenyeji inaanza kesho Alhamisi asubuhi, Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam, Tanzania. Kisha atasafiri hadi Nairobi, Kenya na Kampala, Uganda siku ya Ijumaa, Desemba 20, 2024 ambapo atahitimisha ziara yake ya mataifa hayo matatu.
Katika ziara yake hiyo, Dkt. Motsepe atakutana na Serikali, Uongozi wa Soka na Kamati za Maandalizi za Serikali za Mitaa kutoka nchi hizo tatu.
Ratiba ya shughuli na mikutano inajumuisha kutembelea viwanja vya mechi na mazoezi ambavyo kwa sasa vinafanyiwa ukarabati kabla ya mashindano ya mwaka ujao.
Ziara ya Dkt. Motsepe inakuja nyuma ya ziara ya pili ya ukaguzi wa mataifa matatu mwenyeji iliyofanywa na ujumbe wa Caf mwezi Novemba mwaka huu ambapo viwanja mbalimbali, maeneo ya mazoezi, hoteli, viwanja vya ndege na vifaa vingine vilikaguliwa.
Michuano ya Chan itafanyika Februari Mosi hadi 28, 2024 lakini pia mataifa hayo yataandaa Afcon mwaka 2027.