Pointi 12 tu freshi Ruvu Shooting

Wakati Ruvu Shooting ikihaha kukwepa rungu la kushuka daraja, benchi la ufundi la timu hiyo limesema katika mechi sita zilizobaki wanahitaji japo pointi 12 na kusubiri hatma yao ya kubaki ligi kuu au kucheza Play off.
Hadi sasa timu hiyo ndio inaburuza mkia kwa pointi 17 na kesho Ijumaa itakuwa uwanjani kunyooshana na Mbeya City, mechi ilipigwa Sokoine jijini hapa.
Hata hivyo timu hizo zinakutana ikiwa Ruvu Shooting inakumbuka kutopata ushindi dhidi ya wapinzani hao kwenye uwanja huo na matokeo mazuri kwao ni sare na mchezo uliopita City walishinda bao 1-0 wakiwa ugenini uwanja wa Mabatini Pwani.
Akizungumza leo jijini hapa kocha msaidizi wa timu hiyo, Frank Msese amesema licha ya uhitaji wa ushindi kwenye mechi zilizobaki, lakini hesabu zao ni kuvuna alama 12 kwenye mechi sita walizobakiza.
Amesema wamepitia wakati mgumu kupata matokeo mazuri licha ya timu kucheza vyema, lakini shida imekuwa kwenye sehemu ya ufungaji mabao jambo ambalo wamelifanyia kazi.
"Hata mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar tulitengeneza nafasi nyingi lakini shida ilikuwa ni umaliziaji, kadharika beki haikuwa nzuri ila tumelifanyia kazi na kesho tunaenda kupambana kuanza msako wa pointi 12 kati ya 18 kwenye mechi sita zilizobaki" amesema Msese.
Naye Straika na Nahodha wa timu hiyo, Abdulrahman Mussa amesema matokeo waliyonayo hivi sasa hayachangiwi na hali yoyote ndani au nje ya uwanja isipokuwa ni mpira tu na kwamba wanapambana kujinusuru kushuka daraja.
"Hatuna shida yoyote ni matokeo ya mpira kwa sasa mazungumzo yetu wachezaji ni kuibakiza timu kwenye ligi kuu kama tulivyoikuta, tunajua mechi ya kesho itakuwa ngumu ila hatuna namna nyingine ya kushinda" amesema Mussa.
Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima amesema pamoja na kuwaacha wapinzani hao kwenye msimamo lakini watakuwa makini kushinda kwani hata wao hawapo pazuri.
"Tumetoka kushinda mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar mchezo wa kombe la shirikisho huu ni mchezo mwingine tunahitaji ushindi ili kujiweka pazuri" amesema Mwamlima.