Pesa kiduchu, lakini hutoki

Muktasari:
- Cheki pesa aliyouzwa Luis Suarez na mwenzake Philippe Coutinho. Wote hao walinaswa na Liverpool kwa pesa kiduchu, lakini ilipokuja kuwapiga bei, waliuzwa kwa pesa ndefu kwa sababu ile huduma yao waliokuwa wakiitoa kwenye kikosi hicho kuwa matata kwelikweli.
LIVERPOOL ndo zao. Kwa sasa kila timu inamtaka Mohamed Salah na hakika kama itahitaji huduma yake na kumng’oa kutoka Anfield, basi lazima mkwanja mrefu sana uhusike.
Cheki pesa aliyouzwa Luis Suarez na mwenzake Philippe Coutinho. Wote hao walinaswa na Liverpool kwa pesa kiduchu, lakini ilipokuja kuwapiga bei, waliuzwa kwa pesa ndefu kwa sababu ile huduma yao waliokuwa wakiitoa kwenye kikosi hicho kuwa matata kwelikweli.
Hicho ndicho kitakachotokea kwa Mo Salah kama atanaswa na timu nyingine kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi.
Salah, alinaswa kwa Pauni 34 milioni, lakini ukimtaka kwa sasa, basi jipange na mkwanja unaoanzia Pauni 200 milioni.
Cheki kikosi hiki cha Liverpool kilichonunuliwa kwa pesa ndogo sana, lakini huduma waliyokwenda kutoa huko Anfield ilionekana kama wamewanasa bure kabisa kwa ubora wao.
KIPA
Kwenye kikosi hicho Anfield, kipa aliyenaswa kwa pesa ndogo zaidi ni Mhispaniola Pepe Reina, aliyetua kutoka Villarreal kwa Pauni 6 milioni. Kocha Rafa Benitez alimfanya kipa huyo kuwa chaguo la kwanza na hakika mambo yake yalikuwa matamu na kuwa chaguo la kwanza hadi hapo Brendan Rodgers alipowasili kuinoa timu hiyo.
Reina alishinda mara tatu mfululizo tuzo ya Kipa Bora wa Msimu.
BEKI
Kwenye kikosi hiki, ambacho kitatumikia mfumo wa 4-3-3, kwenye sehemu ya ulinzi, beki wa kushoto ni Andy Robertson, ambaye alinaswa na Liverpool kwa ada ya Pauni 8 milioni tu akitokea Hull City, wakati beki wa kulia ni Alvaro Arbeloa, aliyenaswa kutoka Deportivo La Coruna kwa ada iliyochini ya Pauni 3 milioni.
Mabeki wa kati ni Daniel Agger, aliyesajiliwa kwa Pauni 5.8 milioni na Sami Hyypia, aliyetua Anfield kwa Pauni 2.7 milioni. Hiyo ni safu matata kabisa ya ulinzi, ambayo thamani yake hata Pauni 20 milioni haizifiki.
KIUNGO
Kwenye ile safu ya viungo watatu, Xabi Alonso, atasimama kwenye kiungo ya kukaba na ukweli Mhispaniola huyo kwa huduma yake yote ile hata Real Madrid ikatoa Pauni 30 milioni kumsajili, Liverpool ilimnunua kwa Pauni 10.7 milioni tu. Staa mwingine matata wa gharama nafuu anayeingia kwenye sehemu hiyo ya kiungo ya Liverpool ya bei chee ni James Milner, ambaye alitua Anfield bure bila ya senti yoyote, huku Coutinho, alipata nafasi baada ya usajili wake kuigharimu Liverpool Pauni 8.5 milioni tu ilipomsajili kutoka Inter Milan. Hivi kuna mwenye swali juu ya huduma ya viungo hao kwa kile walichokifanya Liverpool licha ya kuwa wachezaji wa bei nafuu? Hatakuwapo.
FOWADI
Pengine hii ndiyo safu hatari zaidi iliyowahi kutokea kwenye kikosi cha Liverpool pale kwenye ushambuliaji. Hivi vuta hisia, unakuwa na fowadi yenye Salah na Suarez unadhani wapinzani watateseka kiasi gani? Liverpool imebahatika kusajili wachezaji kwa gharama ndogo kisha wanakwenda kuwa wachezaji wakali sana wannapotua kwenye kikosi chao.
Kwenye fowadi ya bei chee, pengine Salah ndiye aliyenaswa kwa pesa nyingi zaidi Pauni 34 milioni, lakini Suarez alinaswa kwa Pauni 22.5 milioni tu kutoka Ajax, wakati staa mwingine hapo ni Raheem Sterling, ambaye baadaye aliuzwa kwa pesa nyingi Manchester City, yeye alitua Anfield kwa Pauni 500,000 tu akitokea QPR. Salah alitokea AS Roma.