Patashika : Kombe la Mabara laitikisa Dunia Brazil

Muktasari:
- Brazil imetua kwenye michuano hiyo kwa tiketi ya wenyeji wakati Hispania ipo hapo kwa sababu ni Mabingwa wa Dunia. Japan ni mabingwa wa Asia, Nigeria ni vinara wa Afrika, Italia imeingia hapo baada ya kutua fainali za Euro 2012.
RIO DE JANEIRO,BRAZIL
HEKAHEKA za Kombe la Mabara zinaanza leo Jumamosi huko Brazil ambapo timu nane za soka ambazo ni mabingwa wa mabara zitatoana jasho.
Timu hizo zinawania ubingwa ambao unaweza kutoa mwongozo wa fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa pia nchini humo mwakani.
Timu zimegawanywa kwenye makundi mawili. Kundi A lina Brazil, Japan, Mexico na Italia huku Kundi B likiwa na timu za Hispania, Uruguay, Tahiti na Nigeria.
Brazil imetua kwenye michuano hiyo kwa tiketi ya wenyeji wakati Hispania ipo hapo kwa sababu ni Mabingwa wa Dunia. Japan ni mabingwa wa Asia, Nigeria ni vinara wa Afrika, Italia imeingia hapo baada ya kutua fainali za Euro 2012.
Italia imechukua nafasi hiyo kwa sababu ni mabingwa wa Ulaya, Hispania tayari walikuwa na nafasi yao kufuatia ubingwa wa Dunia.
Mexico ilishinda Kombe la Concacaf (2011), Tahiti mabingwa wa OFC (2012) na Uruguay ni washindi wa michuano ya Copa America (2011). Makala hii inaangalia nafasi ya kila timu.
8. Tahiti
Tahiti ndio timu inayoshika mkia miongoni mwa timu ninazoshiriki michuano hiyo. Ipo nafasi ya nane kwa kuwa ni vigumu kwa timu ambayo ipo nyuma kisoka kupambana na wababe wa dunia.
Timu hiyo ilifika kwenye michuano hiyo baada ya kuibuka kidedea kwenye michuano ya OFC ya mwaka 2012. Timu inatarajiwa kuongozwa na Marama Vahirua, anayechezea Nancy ya Ufaransa.
Wachezaji wengine wa kikosi hicho hawana uzoefu mkubwa ingawa Alvin Tehau ana uzoefu kiasi.
7. Japan
Hakuna mabadiliko ya maana kwa kikosi cha kocha, Alberto Zaccheroni, tangu walipopata Kombe la Asia mwaka 2011.
Huenda timu hiyo ya Asia isiwe na nguvu kubwa mbele ya kundi ambalo linajumuisha Italia, Brazil na Mexico.
Timu hiyo ina matatizo katika safu ya ulinzi na huenda hilo likawamaliza.
Yasuhito Endo na Makoto Hasebe ndio watakuwa vinara ndani ya kikosi. Awali timu ilijitahidi eneo la beki lakini kuumia kwa Yuto Nagatomo ni pigo kubwa.
Vile vile nyota kama Ryoichi Maeda, Shinji Okazaki, Keisuke Honda na Shinji Kagawa wataonyesha kiwango, hata hivyo itakuwa kazi kubwa kuvuka kwenye kundi lao.
6. Nigeria
Kocha Stephen Keshi amekuwa akiwajaribu wachezaji mara kwa mara katika mechi za karibuni, lakini amefanya mabadiliko kidogo kwenye timu yake ambayo ilitwaa ubingwa wa Afrika mapema mwaka huu.
Vincent Enyeama ni kipa mwenye kiwango cha juu, mbele yake kuna mabeki; Elderson Echiejile, Kenneth Omeruo, Godfrey Oboabona na Efe Ambrose. Keshi anatumia mfumo wa 4-3-3.
Baada ya kuonyesha kiwango cha wastani kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika, Nosa Igieba alitemwa. Lakini Ogenyi Onazi na Sunday Mba wanategemewa kuwasha moto.
Kikosi kitakuwa na John Obi Mikel ambaye anategemea kutamba. Lakini kukosekana kwa Victor Moses na Emmanuel Emenike ni pigo kwa Keshi. Ideye Brown aliyeonekana butu ametolewa na Anthony Ujah amechukua nafasi.
Lakini kikosi hakina ubunifu eneo la kiungo na kukosekana kwa Moses na Emenike mbele ni pigo.
5. Uruguay
Swali gumu linalomkabili kocha, Oscar Tabarez, ni upangaji wa mshambuliaji. Kocha yeyote ambaye ana nyota kama Edinson Cavani, Diego Forlan na Luis Suarez anaweza kuwa njia panda hasa anapokuwa na mfumo wa 4-4-1-1.
Forlan amepunguza uwezo wa kufunga mabao, lakini ana mbinu za ushindi, Cavani naye ni nyota tegemeo wa Napoli na amekuwa akifunga mabao, Suarez naye ni tegemeo la Liverpool.
4. Mexico
Kikosi hicho kwa sasa hakipo vizuri, timu imetoka sare mara nane na kushinda mara moja kwenye mechi za karibuni, hiyo inatoa wasiwasi kama watafika mbali.
Pamoja na hayo, Mexico ni timu ngumu na haifungiki kirahisi. Vilevile timu ina watu wa kusumbua kama vile akina Marvel na Andres Guardado. Javier Hernandez ‘Chicharito’ naye ni nyota wa uhakika wa kuivusha timu yake.
3. Italia
Licha ya kunyanyaswa na Hispania kwenye Euro 2012, Italia bado ni timu ngumu, ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye michuano hii.
Timu ilifumuliwa na kuundwa upya baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 na kocha Cesare Prandelli amepewa vitendea kazi vya kutosha.
Huku kukiwa na washambuliaji wa kutumainiwa, Stephan El Shaarawy na Mario Balotelli, hakuna ubishi kuwa kikosi cha Azzuri kinashitua. Andrea Pirlo atacheza nafasi ya kiungo na Riccardo Montolivo naye anategemewa kufanya vema.
2. Hispania
Ni Mabingwa wa Dunia na Ulaya. Ni timu ya kwanza kupata vikombe vitatu vikubwa mfululizo. Ina wachezaji wapya wakali kama Santi Cazorla, Juan Mata, David Silva na Javier Martinez.
Mabeki Cesar Azpilicueta na Nacho Monreal ni vigumu kuwapita. Ingawa kuna nyota wakali kwa sasa, kuna wakongwe walioanza kuyeyuka.
Kuumia kwa Carles Puyol pamoja na umri kusonga mbele ni ishara mbaya kwa kikosi. Xavi Hernandez bado ni mahiri, lakini hakufanya vizuri kwenye mechi za karibuni.
Mbele napo kuna matatizo, Fernando Torres na David Villa hawapo kwenye viwango vikubwa. Kitendo cha kufunga mabao 25 kwenye mechi 36 za La Liga kimefanya Alvaro Negredo atazamwe sana. Kukosekana kwa Xabi Alonso pia ni pigo kwa Hispania.
1.Brazil
Baada ya kuondoa nuksi kwa kuwafunga Ufaransa ukiwa ni ushindi wa kwanza chini ya kocha, Felipe Scolari, Brazil itatua kwenye michuano hiyo ikijiamini.
Jambo jingine jingine litakalowafanya wawe bora ni ukweli kuwa watakuwa kwenye mazingira ya nyumbani.
Nyota mpya wa Barcelona, Neymar, ataongoza safu ya ushambuliaji, Oscar, Lucas Moura na Hulk nao wanatarajiwa kuwa tishio.
Mabeki, Marcelo na Dani Alves wapo tayari kuondoa hatari mbalimbali langoni. Julio Cesar, Thiago Silva na David Luiz nao wanadaiwa kuwa nyota wa kuogopwa kwenye kikosi kipya cha Brazil.