Pamba waishusha Geita Gold kileleni

Sunday November 22 2020
pamba pic

Mwanza. Pamba FC imechumpa kileleni katika Ligi Daraja la Kwanza kundi B baada ya  kuitandika Geita Gold bao 1-0 katika mchezo wa Ligi hiyo uliopigwa uwanja wa Nyamagana jijini hapa.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani ndani na nje ya uwanja kutokana na kila upande kuhitaji na kutamba kuondoka na alama tatu na wenyeji kutumia vyema dimba lao.

Kabla ya mchezo huo wa raundi ya tano katika Ligi hiyo, Geita Gold ndio walikuwa vinara kwa pointi 12 lakini pia kucheza mechi nne mfululizo bila kupoteza wala kutoa sare yoyote na leo kuambulia kipondo hicho cha kwanza.

Katika mpambano huo, kipindi cha kwanza Pamba walitawala sana dhidi ya wapinzani na kuwafanya kumaliza dakika 45 wakiwa mbele kwa bao moja lililofungwa na James Wilson aliyepiga shuti akiwa nje ya eneo la hatari na kuujaza mpira wavuni.

Kipindi cha pili Geita Gold walipambana kulazimisha mashambulizi kwa wapinzani lakini mabeki wa Pamba walikomaa na dakika ya 67, Jonathan Mwaibindi wa Geita Gold alioneshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu, Berege January na kuwafanya kucheza pungufu.

Pamoja na hekaheka kwa timu zote kushambuliana lakini hadi dakika 90 zinamalizika, Pamba imeweza kubaki na alama tatu muhimu na kufikisha pointi 13 na kuwashusha wapinzani hao waliobaki na alama zao 12 baada ya mechi tano kila timu.

Advertisement

.................................................

Na Saddam Sadick

Advertisement