Pacome nyota imeng’ara Ivory Coast

KIUNGO wa Yanga, Pacome Zouzoua amechaguliwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Ivory Coast, huku akienda kuziba pengo la Ibrahim Sangare anayeichezea Nottingham Forest ya Ligi Kuu England (EPL).
Ivory Coast iliyotwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 hivi sasa iko chini ya kocha Emerse Faé aliyeipa ubingwa huo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Klabu ya Nottingham Forest, Sangare ni majeruhi tangu wikiendi kutokana na majeraha aliyoyapata katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Luton Town ambayo alicheza dakika 90 kumalizika kwa sare 1-1.
Kikosi hicho cha Ivory Coast kilichoitwa siku chache zilizopita hapo awali hakikuwa na jina la Staa huyo wa Yanga, lakini baada ya mabadiliko hayo, Pacome akapata nafasi.
Wachezaji walioodolewa na walioingizwa ni pamoja na Seko Fofana ambaye afasi yake inachukuliwa na Kader Keita, huku Sangare nafasi yake inachukuliwa na Pacome ilhali Evan Ndicka nafasi yake inachukuliwa na Emmanuel Agbadou.
Tangu Pacome atue Yanga hii ni mara yake ya kwanza kuitwa timu ya taifa, akiwa miongoni mwa wachezaji 25 watakaoshiriki katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin.
Mchezaji huyo atatakiwa kuripoti haraka kambini nchini Ufaransa ili kujiandaa na mchezo huo utakaochezwa Machi 23.
Ikumbukwe kuwa kiungo huyo anajiunga na kikosi hicho akiwa na majeraha aliyoyapata katika mchezo wa Ligi Kuu Bara wikiendi iliyopita dhidi ya Azam FC.
Kwenye mchezo huo ambao vinara wa ligi Yanga walifungwa mabao 2-1, Pacome aliumia katika dakika ya 28 na kutolewa ndani ya kipindi cha kwanza akiwa amebebwa akishindwa kutembea na kurudishwa vyumbani.
Baadaye mchezaji huyo alionekana amefungwa bandeji kwenye goti. Katika msimu huu nyota huyo amefunga mabao saba katika mechi 20.