Pacome: Nipo fiti, Naumia sana kutocheza

Muktasari:

  • Pacome aliumia Machi 17, mwaka huu kwenye mechi ya ligi dhidi ya Azam iliyopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na timu yake ikipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 yaliyowekwa nyavuni na Feisal Salum 'Fei Toto' na Djibril Sylla huku lile la kufutia machozi kwa Wananchi likifungwa na Clement Mzize.

Mashabiki wa soka nchini wamemisi maufundi ya kiungo wa Yanga, Muivory Coast Pacome Zouzoua aliyekuwa majeruhi, lakini mwenyewe amefunguka kupona na sasa yupo tayari kurejea uwanjani kuendelea kuipambania timu na kutoa burudani.

Pacome aliumia Machi 17, mwaka huu kwenye mechi ya ligi dhidi ya Azam iliyopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na timu yake ikipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 yaliyowekwa nyavuni na Feisal Salum 'Fei Toto' na Djibril Sylla huku lile la kufutia machozi kwa Wananchi likifungwa na Clement Mzize.

Kabla ya hapo Pacome alikuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga akihusika na mabao 11 kwenye ligi, akifunga saba na asisti nne huku kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga iliishia robo fainali akichangia mabao manne kwa kufunga matatu na asisti moja.

Katika mazungumzo aliyoyafanya na Yanga TV, Pacome amethibitisha kupona na kuwa tayari kwa mechi.

"Naweza kusema niko fiti kwa asilimia mia... Mara kwa mara naendelea na programu anazonipa mwalimu Taibu (Lagrouni), pia nilikuwa nikiendelea na tiba ninazopewa kisha kufanya mazoezi ya gym kwa wiki kadhaa na baadaye programu nyingine za kuweka mwili sawa," amesema Pacome aliyeweka wazi Ligi Kuu Bara ni ngumu zaidi kuliko ya nchini kwao, Ivory Coast.

Kiungo huyo aliyetua Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Asec Mimosas ya nchini kwao, amesema anatamani kucheza kwenye mechi ijayo ya Yanga dhidi ya Tabora United walau kwa dakika 10 hadi 15.

"Niko sawa na taratibu taratibu nikipata nafasi ya kucheza hata kwa dakika chache 10 hadi 15 naamini nitarejea nikiwa imara," amesema Pacome.

Staa huyo ameendelea kueleza namna anavyoumia kutocheza mechi za Yanga zilizopita kutokana na majeraha.

"Kama mchezaji nakosa kitu kwenye timu yangu ninapoona wachezaji wenzangu wanavyoipambania timu na jina langu halipo kwenye makaratasi, pale naumia sana," amesema.

"Na ninapotazama kuwa kuna majeraha hayahitaji mimi kucheza, basi naishia kuumia," amesema Pacome aliyeeleza kuumizwa zaidi baada ya timu yake kutolewa na Mamelodi Sundowns kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu huku akikosa mechi zote mbili.

Kiungo huyo amewashukuru mashabiki wa Yanga kumjulia hali katika namna tofauti wakati wa majeraha yake na kuwaahidi kuwa wapo tayari kuipambania timu hiyo kupata ubingwa wa ligi msimu huu licha ya kuwepo kwa ugumu na ushindani kutoka timu nyingine shiriki.

Yanga inaongoza ligi na alama 62 baada ya mechi 24 ambazo imefunga mabao 55 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12, inatarajia kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho (FA), keshokutwa Jumatano, dhidi ya Tabora United katika hatua ya robo fainali.