Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pacome, Maxi washtua Yanga

PACOME Pict

Muktasari:

  • Pacome na Maxi waliosajiliwa msimu uliopita mikataba yao inaenda ukingoni na kulikuwa na tetesi kwamba mabosi wa Msimbazi walikuwa wakiwapigia hesabu ili kuhakikisha wanavuka mtaa kutua Simba, jambo lililowafanya vigogo wa Jangwani kukimbizana kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa.

ACHANA na stori inayotrendi kwa sasa juu ya Yanga kugomea kucheza mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani zao, Simba, ikisisitiza tena kwamba haina mpango wa kucheza mechi hiyo hata kama itapangwa na Bodi ya Ligi, lakini kuna mambo mbalimbali yanayohusiana na mastaa wa timu hiyo.


Tayari Yanga imeshakata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kutokana na nafasi iliyopo kwa sasa, na mabosi wa timu hiyo wameishaingia chimbo kuweka mambo sawa ili mashindano yatakapoanza chama hilo likiwashe na kurejesha heshima yake ngazi ya kimataifa.


Huku nyuma, kama kuna shabiki aliyekuwa akiamini Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wanatimka Yanga kwa vile mikataba waliyonayo kwa sasa inamalizika mwisho wa msimu huu, basi pole yao kwani mabosi wa klabu hiyo wameamua kufanya kweli kuhakikisha nyota hao wa kikosi cha kwanza hawaendi kokote, huku wakishtua kwa kusaini mikataba mipya.


Pacome na Maxi waliosajiliwa msimu uliopita mikataba yao inaenda ukingoni na kulikuwa na tetesi kwamba mabosi wa Msimbazi walikuwa wakiwapigia hesabu ili kuhakikisha wanavuka mtaa kutua Simba, jambo lililowafanya vigogo wa Jangwani kukimbizana kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa.


Mabosi hao wa Yanga wameamua kumaliza mambo kiutu-uzima kwa kuwaita mezani wachezaji hao na kuwaongezea mkataba wa miaka miwili kila mmoja, ili kuendelea kukipiga katika kikosi hicho.

Maxi aliyesajiliwa kutoka AS Maniema ya DR Congo na Pacome aliyetokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast walisainishwa mikataba wa miaka miwili mara walipotua Jangwani ambayo inamalizika mwisho wa msimu huu.

Mmoja wa viongozi wa Yanga, aliliambia Mwanaspoti kuwa, tayari wachezaji hao wameshasaini mikataba mipya baada ya kufanya nao mazungumzo kwa muda mrefu wakishirikisha menejimenti inayowasimamia.

"Pacome bado ataendelea kuwa mchezaji wetu kwa miaka mingine miwili zaidi, baada ya msimu huu kumalizika, isingekuwa rahisi kuachana na mchezaji mwenye kipaji kikubwa kama huyu," alisema bosi huyo wa juu wa Yanga na kuongeza;

"Kifupi haikuwa ishu ngumu kumbakisha, mchezaji mwenyewe alikuwa na amani ya kuendelea kuitumikia Yanga, ameshasaini mbele ya uongozi unaomsimamia sasa tunaangalia mbele zaidi. Ili uwe na timu lazima kuhakikisha unawabakiza wale wachezaji wako wazuri na wakubwa, Yanga haiwezi kuwapoteza wachezaji wake bora labda iamue kuwauza."

Mapema msimu huu kulikuwa na presha kubwa kwa Pacome akitakiwa na klabu tatu za Kaizer Chiefs, Simba na Azam FC, ambazo kwa nyakati tofauti zilikuwa zinapiga hesabu za kumng'oa Yanga.

Ndipo Yanga ilipoamua kukaa mezani na mchezaji mwenyewe kwanza, baadaye ikamalizana na uongozi wake kwa makubaliano ya kumuongeza mkataba wa miaka miwili rasmi.


ISHU YA MAXI

Hapo awali Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa, Simba ilikuwa na hesabu kali za kumsajili Maxi na bosi mmoja alipiga simu DR Congo akiulizia mkataba halisi wa mchezaji huyo, hatua iliyowashtua Yanga.

Wakati Simba ikisubiri majibu, uamuzi wa mwisho yulifanyika baada ya bosi mkubwa wa klabu ya AS Maniema, kumaliza kila kitu akiwaambia wasaidizi wake ndani ya klabu hiyo kuwa, hatma ya kiungo huyo kuondoka ndani ya Yanga labda itokane na timu hiyo kushindwana.

Maniema inayomilikiwa na Jenerali Amissi Kumba, aliyetoa msimamo huo akisema Yanga ni klabu rafiki na kufanya mazungumzo ya kumweka sokoni Maxi ni kama kuwakosea.

Hivyo, Yanga haikupata tabu kufanya mazungumzo ya kumuongeza mkataba Maxi, kwani tayari walishakuwa na uhakika naye tangu Januari.


REKODI ZILIVYO

Yanga ndio kinara hadi sasa, ikishika namba moja katika msimamo wa ligi, ikiwa imecheza mechi 26, imeshinda 23, sare moja na kupoteza mbili ikiwa pointi 70.

Mastaa hao wamekuwa wachezaji muhimu wa muda wote msimu huu, kwani wamekuwa wakipata namba chini ya makocha watatu walioifundisha Yanga msimu huu kuanzia Miguel Gamondi, Sead Ramovic na sasa Miloud Hamdi.

Rekodi zinaonyesha Maxi amecheza mechi 19, akitumia dakika 1,102 na kufunga mabao manne akiasisti manane, wakati Pacome ametumika katika mechi 21 kwa dakika 1,165, akifunga mabao tisa na kuasisti mara nane pia.