Pablo aahidi kuwafunga Arrows

Friday November 26 2021
Pablo PIC
By Ramadhan Elias

KOCHA mkuu wa Simba, Mhispania Pablo Franco amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Red Arrows ya Zambia huku akiahidi ushindi.

Kikosi cha Simba leo jioni kimejifua kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kujiandaa na mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu mechi itakayopigwa Jumapili Novemba 28 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Baada ya kumalizika kwa mazoezi kocha Pablo alizungumza na waandishi wa habari na kufunguka kuwa wamejipanga vizuri na wanatarajia ushindi kwenye mchezo huo.

“Kiukweli nimefurahi kuwa hapa, mbele yetu tunamchezo na Red Arrows ni mechi ngumu lakini tumejipanga kucheza vizuri na kushinda.

Timu inaendelea vizuri, kila siku wachezaji wanaongeza kitu na maendeleo ya mmoja mmoja nayaona hivyo Jumapili tutakuwa na mchezo mzuri na wa kuvutia,” alisema Pablo.

“Nimewaona mashabiki wa Simba, wanaipenda sana timu na wanataka ushindi na mimi kwa kushirikiana na benchi la ufundi tupo hapa ili kuifanya timu ipate matokeo mazuri hapo Jumapili na katika kila mechi ijayo,” amesema.

Advertisement

Aidha Pablo alizungumzia kikosi chake ambapo aliweka wazi kuwa  bado anatafuta kikosi cha kwanza hivyo kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi chake hadi pale atakapojidhihirisha.

“Kila mechi ni tofauti na tutafanya mabadiliko ya wachezaji kwenye kila mechi kwani wachezaji wetu wote ni bora na tunafanya hivyo ili kuwapa muda wa kupumzika pia kuangalia nani na nani wanatufaa zadi lakini kiujumla tuko vizuri,” amesema Pablo.

Naye Nahodha wa timu hiyo John Bocco kwa niaba ya wachezaji amesema;

“Tupo timamu, mazoezi yanaendelea vizuri na tupo kwenye morali ya juu. Tunajua tunaenda kucheza na timu ngumu lakini tumewasoma wapinzani wetu na tupo tayari kupambana na kupata ushindi kwenye mchezo hapo Jumapili,” amesema Bocco.

Simba iliingia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi uliopita.

Advertisement