Ozil, Samatta wachemka dabi

MBWANA Samatta na Mesut Ozil wamechemka kwenye mchezo wa dabi huko Uturuki ambako imeshuhudiwa Fenerbahce ikikumbana na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Galatasaray kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Aliyeamua matokeo ya ushindi kwenye mchezo huo wa dabi ambao unafahamika zaidi huko Uturuki kama ‘Intercontinental Derby’ ni nyota wa Kimataifa wa Misri, Mostafa Mohamed ambaye anaichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Zamalek. Katika mchezo huo wa mahasimu kwenye soka la Uturuki, Samatta alipata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza cha Fenerbahce huku Ozil akiwa benchi.
Kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza nahodha huyo wa Taifa Stars alionekana kudhibitiwa vilivyo na nyota wa zamani wa West Bromwich ya England na Betis ya Hispania Ryan Donk, alipokuwa akijaribu kumkimbia alikumbana na Marcao Teixeira ambaye alikuwa akiondoa mipira yote ya hatari.
Donk alikuwa akitembea na Samatta huku Teixeira akionekana kuwa huru hivyo ilikuwa rahisi kwake kuwa wa kwanza kuifikia mipira baada ya purukushani za nahodha huyo wa Taifa Stars kupambana ‘kugongana’ na aliyekuwa anakula naye sahani moja. Zilikuwa hesabu nzuri kwa Galatasaray.
Kocha wa Fenerbahce, Erol Bulut alistuka kipindi cha pili na kumuingiza Ozil dakika ya 63 ili akaongeze nguvu huku ikimbidi, Enner Valencia aliyekuwa akitokea pembeni asogee juu ambako alisimama Samatta.
Mohamed aliitanguliza Galatasaray dakika ya 54 hivyo mabadiliko hayo yalilenga kusaka bao la kusawazisha lakini hayakuonekana kuwa na matunda ikabidi Bulut afanye mabadiliko mengine ya haraka kwa kuwatoa Samatta na Valencia huku nafasi zao wakiingia, Papiss Cisse na Sinan Gumus. Licha ya mashambulizi kadhaa ambayo walikuwa wakiyafanya mwishoni mwa kipindi cha pili, Galatasaray walikuwa imara na kuondoka na pointi tatu.