Fiston ashtukia jambo Yanga

STRAIKA mpya wa Yanga, Fiston Abdulrazack amecheza dakika 78 za kwanza ndani ya Yanga katika mchezo wa kirafiki ambao timu yake ilipoteza kwa mara ya kwanza msimu huu, lakini jamaa akasema wala hakuna shida kuna kitu ameshagundua ndani ya timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada Yanga kupoteza dhidi African Sports ya Tanga kwa bao 1-0 juzi ukiwa ni mchezo wa kirafiki, Fiston aliwatuliza mashabiki na kuwaambia ni mapema kuanza kuona ubora wake kwa sasa ila muda mchache ujao watapata burudani atakapoanza kutupia nyavuni.
Fiston aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo na kutua hivi karibuni na kujifua na wenzake kambini ambako amekuwa akisifiwa kwa kutupia sana nyavuni, kabla ya jana kushindwa kufurukuta katika mchezo wa kwanza wa kirafiki uliomtoa hadharani.
Hata hivyo, straika huyo aliwayewahi kuwika kwenye soka la nchi za Afrika Kusini na Misri sambamba na kuichezea timu ya taifa ya nchi yake ya Burundi, alisema bado viungo wa timu hiyo hawajamjulia ni aina gani ya pasi anazotaka ndio maana ameshindwa kutakata juzi usiku.
“Mimi naona tumecheza vizuri, ni mchezo wa kwanza naona kuna mambo mazuri yatakuja, nilichoona bado hatujaweza kucheza kwa uelewano kati yangu na viungo hii ni mechi ya kwanza kwangu katika timu hii,” alisema Fiston na kuongeza;
“Viungo hawajajua sana aina ya pasi ambazo naweza kuzitumia kufunga ni suala la muda tukishazoeana kidogo tu, nadhani mambo mengi yatabadilika binafsi sina wasiwasi kabisa tena nimefurahia mwanzo huu ingawa tulipoteza.”
Fiston alisisitiza kwa jinsi alivyowaona viungo wa Yanga na mawinga wa timu hiyo anaamini kama hatakuwa na shida kumkosesha kucheza basi ana uhakika anaweza kuja kufunga karibu kila mchezo.
“Mimi najijua, mimi sio mchezaji mdogo nimewaona wachezaji wenzangu kuna niliowakuta na kuna wengine wamekuja tena ninaimani kubwa na aina ya wachezaji waliopo hapa Yanga, kuna mawinga wazuri na hata viungo kilichobaki hapa ni kuelewana tu ili mashabiki wetu waweze kufurahi,” alisema Fiston aliyeshika nafasi ya pili ya ufungaji katika fainali za Afcon 2019 zilizofanyika Misri na kuongeza;
“Mimi nitafunga sana hapa Yanga kwa jinsi ninavyowaona wachezaji wenzangu bora kuanzia viungo wa kati,mawinga a hata washambuliaji wenzangu nikiangalia ubora wao naweza kusema nitafunga karibu kila mechi.”
MSIKIE KAZE
Kocha aliyemleta Fiston, Cedric Kaze akizungumzia kiwango cha mshambuliaji wake huyo alisema wala hana wasiwasi na raia mwenzake huyo wa Burundi na katika mchezo wake wa kwanza ameonyesha kitu huku akitaka apewe muda.
“Fiston amecheza vizuri hii ni mechi yake ya kwanza kwa alivyocheza sisi kama makocha hakuna ambacho tunaweza kusema amekosea ni suala la muda. Muda bado upo wa yeye kuweza kuonyesha thamani yake,” alisema Kaze.