Onyango asaini mkataba mpya Simba

Beki wa kimataifa wa Kenya, Joash Onyango ameongeza mkataba Simba SC baada mkataba wake wa awali kumalizika mwisho wa msimu huu.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya  Simba zinasema kuwa pande zote mbili zimefikia makubaliano na Onyango atakuwa Simba kwa misimu miwili ijayo huku baadhi ya matakwa ya beki huyo hayakutekelezwa ingawa mkataba wake uliboreshwa na kumridhisha.

Tangu alipojiunga na Simba, Onyango amecheza sehemu muhimu ya timu  akiwa kama beki wa kati ambapo amekuwa akisaidiana na beki kisiki kutoka Congo, Eneck Inonga, Kennedy Juma pamoja na Pascal Wawa ambaye kwasasa hatokuwepo kwenye kikosi cha Wanamsimbazi msimu ujao.

Hata hivyo kulikuwa na hofu juu ya mustakabali wa Onyango baada ya kukosa mechi mbili za mwisho za Simba dhidi ya Mbeya City na KMC huku Mei mwaka jana, vigogo wa Afrika Kusini, Orlando Pirates, walionyesha nia ya kutaka kuwasajili wachezaji hao na aliyekuwa Msemaji wa Simba wakati huo, Haji Manara (sasa Yanga SC) akadai kitita cha Sh100 milioni.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 anakuwa mchezaji wa pili ndani ya klabu ya Simba kuongezewa mkataba ambao wa kwanza ni Aishi Manula ambaye aliongezewa mkataba siku chache zilizopita huku Rally Bwalya, Bernard Morrison na Pascal Wawa wakiondoka klabu hapo.