Okrah: Hizi ndo mechi zangu

NYOTA mpya wa Simba, Augustine Okrah amesema kati ya mechi anazozisubiri kwa hamu ni Dabi ya Kariakoo na kufafanua yeye ni mtu wa mechi hizo na kiu yake imeongezeka baada ya kuiona Yanga.

Simba na Yanga zinavaana leo katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Okrah litakuwa pambano lake la kwanza la Kariakoo Derby, lakini alisema sio mgeni wa mechi kama hizo.

Kiungo mshambuliaji huyo kutoka Ghana alisema amecheza dabi mbalimbali kubwa akiwa kwao Ghana na Sudan na kufafanua mechi zinazomtambulisha kwa urahisi mchezaji hasa akicheza kwa kiwango bora.

Alisema wachezaji wapya wa Simba na waliokuwepo msimu uliopita wanaitaka mechi hiyo kutokana na kutamani kupata ushindi ili kuchukua taji lao la kwanza msimu huu.

“Tuliiona Yanga katika mechi ya kirafiki ikicheza na Vipers, ni timu kubwa na nzuri kama nikieleza mabeki gani wapo vipi maana yake nitawafanya wajirekebishe kabla ya kukutana nasi ila nikueleze Simba tunakwenda kuonyesha kiwango bora dhidi yao na kupata ushindi,” alisema Okrah aliyesajiliwa msimu huu kutoka Becham United ya Ghana.

“Nilikueleza awali hii sio dabi yangu ya kwanza, nimekuwa mchezaji aliyezoea mechi za aina hii, na nina hamu kubwa ya kuwepo kikosini dhidi ya Yanga, itakuwa mara yangu ya kwanza hapa lakini hakuna mechi rahisi katika dabi, ila tumejiandaa vizuri na kuweka mipango sahihi ili tupate matokeo bora.”

Alisema kwa namna walivyokuwa kambini Misri na sasa jijini Dar es Salaam ni wazi wachezaji wameiva kwa ajili ya kuanza msimu na kuwatoa hofu mshabiki kwa kuwaambia; “Simba hii mpya ni tofauti kabisa.”