Nyota 7 waiweka Simba njia panda

Paul Kiongera
Muktasari:
Wachezaji hao wakiongozwa na chipukizi Ibrahim Ajib, Hassan Kessy na Mrundi Emery Nimubona ambao mikataba yao inaelekea ukingoni huku viongozi wa Simba wakisuasua kumalizana nao mapema.
SIMBA ipo kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 57, ingawa ishatolewa kwenye mbio za kuwania ushiriki wa michuano ya kimataifa kupitia Kombe la FA, lakini klabu hiyo ipo hatarini kupoteza nyota wake saba kama wasipokuwa makini.
Wachezaji hao wakiongozwa na chipukizi Ibrahim Ajib, Hassan Kessy na Mrundi Emery Nimubona ambao mikataba yao inaelekea ukingoni huku viongozi wa Simba wakisuasua kumalizana nao mapema.
Mbali na Ajib anayeshikilia nafasi ya pili kwa ufungaji mabao katika klabu hiyo nyuma ya Mganda, Hamis Kiiza, wengine wenye mikataba inayoishia ni nahodha Mussa Hassan Mgosi, Mkenya, Paul Kiongera, kipa Peter Manyika na kipa aliyepo kwa mkopo Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif ‘Casillas’.
Habari za ndani kutoka Simba zinasema kuwa Ajib aliyefunga mabao 9 pamoja na Kessy mpaka sasa hawajasaini mkataba mpya, ingawa mazungumzo ya awali yameanza, ila kama mabosi wa Msimbazi wakizubaa wanaweza kuwakosa hivi hivi.
Beki Mrundi, Nimubona aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja huku mwingine kwa makubaliano ya kupewa mkataba mwingine endapo atafanya vizuri ila mpaka sasa hakuna mazungumzo yaliyofanyika juu ya kumpa mkataba mpya sawa Mgosi, kipa Peter Manyika na Kiongera ambaye aliwahi kunukuliwa akidai kuwa hataki tena kubaki Simba.
Kwa upande wa Casillas aliyebakisha miezi miwili katika mkataba wake akiichezea kwa sasa Mtibwa Sugar ameshaeleza kuwa hana mpango wa kurudi Msimbazi hata kwa fimbo kutokana na kutoridhishwa na mambo aliyokutana nayo aliposajiliwa.
Ajib afunguka
Mwanaspoti lilimtafuta Ajib lakini aliishia kusema: “Mimi sifahamu lolote, mambo ya mkataba anashughulikia meneja wangu ambaye kwasasa yupo nje ya nchi, mimi natumwa kucheza tu ndiyo kazi yangu, meneja ndiye anaweza kufahamu hilo na kulizungumzia.”
Japo Mwanaspoti inafahamu meneja wake hayupo nje ya nchi, alikumbwa na tatizo la kisheria ambalo limemuweka ndani mpaka sasa.
Casillas agoma
Kwa upande wa Casillas amekiri mkataba wake Simba umebaki miezi miwili tu na amesema, hafikiri kusaini kwa mara nyingine klabuni hapo na anaangalia mbele.
“Kweli mkataba Simba unakwisha karibuni kama miezi miwili tu, lakini sifikirii kusaini hapo, sitaki naangalia mbele, ni kubaki Mtibwa au kwenda timu nyingine.”
“Kuna timu nyingi zimeshaanza kunipigia simu zikinihitaji, nitaangalia itakavyokuwa,” alisema Casillas ambaye kabla ya kwenda Simba, akiwa Mtibwa aliwahi kuwa kipa bora ligi kuu bara.
Aveva anena
Hata hivyo Rais wa Simba, Evans Aveva aliposakwa alifafanua juu ya mikataba ya wachezaji hao alikiri wengine mikataba imeisha, ila kwa Ajib alikataa akidai bado ni mchezaji wao halali.
“Ajib bado ana mkataba Simba, nadhani unaisha mwakani au 2018, hao wengine tunasubiri taarifa ya Kocha Mayanja (Jackson) na benchi la ufundi kuamua hatma yao,” alisema Aveva.
Imeandikwa na Mwanahiba Richard, Doris Maliyaga na Olipa Assa.