Nyoni aiota Top 5, Kabunda amtaja Mgunda

Muktasari:
- Namungo inashika nafasi ya tisa kwa sasa ikiwa na pointi 31 kwa kucheza mechi 27 ikishinda nane, sare saba na kupoteza 12 na kama itashinda mechi tatu ilizobakiza itaweza kufikisha alama 40 ambazo zinaweza kuwaingiza katika Tano Bora inayoshikiliwa kwa sasa na Tabora United yenye pointi 37.
WAKATI nyota mkongwe wa Namungo, Erasto Nyoni akiweka bayana anavyotamani kuona timu hiyo ikipambana ili imalize katika Tano Bora ya Ligi Kuu Bara, mshambuliaji anayekipiga kwa Wauaji wa Kusini hao, Hassan Kabunda amemtaja kocha Juma Mgunda kama aliyewarejesha katika mstari.
Namungo inashika nafasi ya tisa kwa sasa ikiwa na pointi 31 kwa kucheza mechi 27 ikishinda nane, sare saba na kupoteza 12 na kama itashinda mechi tatu ilizobakiza itaweza kufikisha alama 40 ambazo zinaweza kuwaingiza katika Tano Bora inayoshikiliwa kwa sasa na Tabora United yenye pointi 37.
Licha ya kwamba Tabora inaonekana ni kama kauzibe kwa Namungo kwa pointi ilizonazo kwa sasa ikisaliwa pia na mechi tatu, bado nyota huyo wa zamani wa Vital’O, Azam na Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa, wachezaji wamejipanga kupambana kushinda mechi zilizosalia.
Timu hiyo imesaliwa mechi dhidi ya Mashujaa, JKT Tanzania na KMC na Nyoni mwenye mabao manne na asisti tatu hadi sasa katika Ligi Kuu alisema: “Nafahamu presha kubwa iliyopo katika mechi za mwisho zilizobeba uamuzi wa ubingwa, kujikwamua kushuka daraja na kumaliza katika nafasi za juu, inakuwa ngumu kwa wachezaji kupambana hadi tone la mwisho.
“Ni hamu ya kila mchezaji wa Namungo kumaliza kwa kishindo ili kuzipata pointi 40 zitakazotusaidia kuishi katika ndoto zetu za kumaliza Top 5 katika msimamo wa Ligi Kuu.”
Aliongeza kuwa, ligi ya msimu huu ni ngumu, lakini imesaidia kuwapa nafasi wachezaji kuonyesha ubora wao, utakaofanya wafaidike na vipaji vyao, endapo tu wakiamua kujitoa kwa kadri wawezavyo.
“Ni kawaida yangu ninapokaa na vijana kuwaambia nidhamu na kujituma hakuwezi kuwaangusha, ila jambo la msingi zaidi ni mtazamo unabakia wao kuyafanyia kazi maelekezo ya makocha ili kula matunda ya vipaji vyao,” alisema Nyoni kinara wa kucheza mechi nyingi za timu ya taifa, Taifa Stars.
Alisisitiza kujituma kwa chipukizi ni faida kwa timu ya taifa kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
“Wachezaji wana vipaji vikubwa, waongezee bidii na nidhamu itakayowafanya kudumu katika viwango bora, kwani siyo miujiza ni muendelezo wa mazoezi na kuzingatia miiko ya soka.”
KABUNDA KAONGEA
Katika hatua nyingine, mshambuliaji wa Namungo, Hassan Kabunda amemtaja kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda kuwa ni mtu aliyefanya kazi kubwa ya kuhakikisha timu hiyo inasalia Ligi Kuu baada ya kurejesha morali ya wachezaji waliokuwa wamekata tamaa kwa mechi za awali za msimu huu.
Kabunda anayeitumikia Namungo kwa msimu wa tatu tangu aliposajiliwa kutoka KMC aliichezea kwa misimu minne, alisema Mgunda anafanya kila kitu hasa kutoa hamasa kwa wachezaji kuisaidia timu hiyo.
“Mchango wake upo mkubwa tena sana muhimu lengo kuu linakuja kwetu sisi lazima kupambana kuhakikisha tunabaki maana ni wajibu wetu wachezaji kupambania timu isihuke daraja,” alisema Kabunda anayemiliki bao moja hadi sasa katika Ligi Kuu.
Alisema kwa mechi tatu zilizosalia ni mkakati wa kuhakikisha wanapata pointi tatu kwa kila mchezo ili kupunguza presha ya kucheza play-off mwishoni mwa msimu.
“Sio nafasi mbaya sana kwa sababu malengo kwa sasa ni kubaki, inamaananisha tunayo nafasi nzuri ya kufanya vizuri licha ya ugumu wa mechi zilizosalia, ila niseme wazi kocha Mgunda amesaidia mno kurejesha morali ya wachezaji waliokatishwa tamaa msimu ulioanza.”
Tangu aanze kazi Namungo, Oktoba 20, 2024 akimpokea Mwinyi Zahera, kocha Mgunda ameiongoza timu hiyo katika mechi 15, wakishinda tatu, sare sita na kupoteza nane na hivyo kuvuna pointi 15.