Nyambui humwambii kitu kwa Yanga

Muktasari:
Nyambui ni miongoni mwa wanamichezo tofauti na soka ambao wamekuwa wawazi juu ya mapenzi yao na klabu za Simba au Yanga, wengine baadhi ni bondia Francis Cheka na Mada Maugo ambao ni Simba kindaki ndaki.
LICHA ya kukiri kuwa ni shabiki kindakindaki wa Yanga, mwanariadha nyota wa zamani nchini, Suleiman Nyambui ameeleza kukubali kiwango cha kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto'.
Nyambui mmoja wa wanariadha wawili Watanzania waliowahi kupata medali za Olimpiki amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa Fei Toto ni mchezaji wa kimataifa, sema hajaamua.

"Fei Toto ni mchezaji ambaye akiamua anaweza kufika hatua ya Mbwana Samatta au hata zaidi, sema hajaamua," amesema Nyambui na kufafanua
"Huyu mchezaji anajua mpira, ingawa hajawa 'serious' na kipaji chake, siku akisema sasa nataka kucheza, ni mchezaji wa levo nyingine kabisa,".
Nyambui ambaye baada ya kustaafu kukimbi alikuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kisha kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha ya nchini Brunei, amekiri kuwa shabiki mnazi wa Yanga.
"Nilianza kuipenda tangu mwaka 1974, wakati ule nilikuwa nikivutiwa mno na kiwango cha Sunday Manara alikuwa ni mchezaji aliyejituma sana," amesema.

Nyambui anasema wakati huo anaanza kuipenda Yanga alikuwa mwanariadha nyota wa timu ya taifa na wakati huo walikuwa wakiingia uwanjani bure, wakitokea kambini kwenye nyumba zilizokuwa pembezoni mwa uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).
"Nakumbuka kuna mechi Yanga ilicheza na timu kutoka Uingereza, Manara alikokota mpira kwenye mstari wa chaki, mzungu kila akijaribu kumzuia hamuwezi, unaona vumbi la chaki tu.
"Ule mpira haukutoka nje na Manara akatoa pasi ya bao, alikuwa ni mchezaji ambaye alifanya nizidi kuipenda Yanga hadi leo,".
Licha ya unazi wake Yanga, Nyambui amesema alikuwa akimpenda nyota wa Simba wakati ule, Abdallah Kibaden ambaye japo alikuwa mwembamba lakini alikuwa na stamina na alijua kutawala uwanja.
"Alikuwa hatulii uwanjani, mchezaji wa timu pinzani akijaribu kumchezea rafu, Kibadeni anaruka au kumkwepa, nilikuwa natamani sana wakati ule awe mchezaji wa Yanga, lakini haikuwezekana," amesema.