Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Debora upepo umebadilika ghafla

Muktasari:

  • Nyota huyo mzaliwa wa Jiji la Luanda, Angola aliwakosha mashabiki wa Simba kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali za kiungo, ikiwamo namba 6 na 8 na ule moto alioanza nao siku ya Simba Day alipofunga bao moja kwa shuti kali la mbali na kuwakuna Wanasimba.

KATI ya sajili zilizobamba msimu huu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara katika kikosi cha Simba, basi ilikuwa ni ule wa kiungao Debora Fernandes Mavambo aliyetua akitokea Mutondo Stars ya Zambia kwa mkataba wa miaka mitatu kutokana na mashabiki kuwa na matumaini makubwa naye.

Nyota huyo mzaliwa wa Jiji la Luanda, Angola aliwakosha mashabiki wa Simba kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali za kiungo, ikiwamo namba 6 na 8 na ule moto alioanza nao siku ya Simba Day alipofunga bao moja kwa shuti kali la mbali na kuwakuna Wanasimba.

Hata hivyo, licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika michezo michache aliyoicheza mwanzoni mwa msimu, Debora alionekana kupoteza nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Simba.

Hii ilitokana na ushindani mkubwa katika eneo la kiungo na wachezaji kama Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma na Yusuph Kagoma wanapambana kuhakikisha wanapata nafasi ya kucheza.

Licha ya ubora wake wa kuanzisha mashambulizi, lakini kwa siku za hivi karibuni amekuwa akipoteza mipira na pasi zake hazifiki.


USHINDANI ULIVYO

Eneo analocheza Mavambo wapo nyota watatu, Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin na Yussuf Kagoma aliyeingia msimu huu akisajiliwa kutokea Singida Black Stars.

Mwanzoni mwa msimu ambao Simba ilifanya mabadiliko makubwa ya usajili kuanzia wachezaji, kocha na benchi la ufundi kwa jumla.

Kocha Fadlu Davids alianza kumtumia zaidi Mavambo wakati ambao bado mgeni kwenye ligi ya Tanzania lakini ghafla upepo ukabadilika kwa staa huyo kuonekana ni kawaida kukaa benchi.

Sasa Fadlu anamtumia zaidi Kagoma ambaye kwenye eneo hilo ameonekana kuwa bora zaidi kwa siku za  hivi karibuni akicheza na Ngoma.

Kagoma ana uwezo wa kumiliki mpira, kupiga pasi ndefu na fupi kwa usahihi, na kufanya kazi ya kukaba kwa ufanisi na hilo linamfanya kuwa sehemu muhimu ya safu ya kiungo na kupewa nafasi kwenye kikosi hicho.

Sifa kubwa ya Ngoma ni mzuri wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma hadi mbele kwa washambuliaji, uwezo wake wa kupiga pasi ndefu na fupi kwa usahihi zinamfanya aendelee kuaminiwa kwenye kikosi hicho.

Hata hivyo, data zinaonekana kumbeba zaidi Ngoma kwani amecheza mechi 19 za Ligi Kuu, dakika 1339 hana asisti akifunga mabao matatu.

Kagoma amecheza mechi 12, dakika 760 akiwa hajafunga bao wala asisti, Mzamiru akicheza saba, dakika 240 akiwa hajafunga bao na hana asisti, wakati huo Mavambo amecheza jumla ya mechi 18, dakika 1017, akifunga bao moja na hana asisti.


WALICHOSEMA WAKONGWE

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Mohamed Banka anaona kinachombeba Kagoma na Ngoma ni pacha nzuri: “Ngoma anautumia vyema uzoefu wake kumpa maelekezo Kagoma ambaye bado ni kijana ana kasi ya kufika katika maeneo kwa muda sahihi.”

Mchezaji mwingine wa zamani timu hiyo, Emmanuel Gabriel anasema:” Mavambo bado ni mchezaji mzuri, anapaswa kuongeza utulivu zaidi kuhakikisha anapopiga pasi zinakuwa zinafika, ndiyo maana wakati anaanza kucheza Ligi Kuu kila mtu alipenda anachokifanya, pia pacha ya Ngoma na Kagoma inafanya vizuri.”