Nyamagana sasa ng’aring’ari

Muktasari:
Kuna matukio kadhaa yaliyotokea kwenye uwanja huo wa jijini hapa kiasi kwamba hata ulipotelekezwa na mamlaka uliwafanya mashabiki wa soka kusononeka kwa kuona inakuwaje?
UWANJA wa Nyamagana una historia ndefu katika soka la Tanzania, kwa wanaokumbuka mwaka 1974 lilipigwa pambano la kihistoria la watani wa jadi Simba na Yanga na Vijana wa Jangwani kushinda mabao 2-1.
Kuna matukio kadhaa yaliyotokea kwenye uwanja huo wa jijini hapa kiasi kwamba hata ulipotelekezwa na mamlaka uliwafanya mashabiki wa soka kusononeka kwa kuona inakuwaje?
Taarifa kwamba ulikuwa kwenye mipango ya kukarabatiwa ulitoa faraja kwa mashabiki, lakini zilipita zaidi ya siku 800 bila kufanyiwa chochote na kuzua maswali mengi, lakini majibu yamepatikana.
Uwanja huo unapendeza sasa baada ya kuwekwa nyasi za bandia na kuanza ukarabati mwingine ambao utaufanya uwe na mwonekano mpya na Mwanaspoti linakuletea hatua kwa hatua katika kuelekea kwenye Nyamagana mpya.
HAIKUWA RAHISI
Uwanja huo ambao unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa wamiliki wake mwishoni mwa mwezi huu ukarabati wake ulisimama kwa karibu miaka miwili na ushei tangu ulipoanza kukarabatiwa.
Hii ilitokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukosa gharama za kutoa nyasi za bandia zilizokuwa zimekwama bandarini Dar es Salaam. Hata hivyo, kuliibuka maswali mengi, ikiwamo ilikuwaje Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ukarabatiwe na kuwekwa nyasi bandia mapema kuliko Nyamagana uliokuwa umeanza kuelezwa ulikuwa ufanyiwe hivyo kabla.
Yakazuka madai kwamba Kaitaba iliwahishwa kwa sababu Rais wa TFF, Jamal Malinzi anatokea huko akiwa kama Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa huo wa Kagera, lakini madai hayo yalikanushwa na kuelezwa tatizo ni fedha.
Hata hivyo, baada ya kelele nyingi hatimaye nyasi hizo zilitolewa bandarini na mwishoni mwa mwezi uliopita zoezi la kuweka nyasi bandia kwenye uwanja huo wa Nyamagana lilianza na Novemba 30 utakabidhiwa rasmi ili kuanza kutumika tena.
HADI BUNGENI
Suala la kukwama kwa uwanja wa Nyamagana lilifikishwa hadi bungeni katikati ya mwaka huu baada ya Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, kuulizwa swali lililojibiwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura.
Waziri alinukuliwa akisema kuwa mradi wa uboreshaji wa Uwanja wa Nyamagana wa kuweka nyasi bandia ulianza mwaka 2014, ukiwa na thamani ya Dola za Marekani 737, 886 ambazo ni sawa na Sh 1.1Bilioni.
Alisema Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), lilitoa msaada kwa TFF kiasi cha Dola za Marekani 618,946 ambazo ni sawa na Sh 1 bilioni na Halmashauri ya Nyamagana ilichangia Dola za Marekani 118,943 sawa na Sh192 milioni. Waziri alidokeza kuwa nyasi hizo bandia zimegharimu tozo kiasi cha Dola za Marekani 100,121.93 sawa na Sh220 milioni ikijumuisha kodi ya gharama ya kuingiza mzigo na VAT.
FURAHA TUPU
Kuwekwa kwa nyasi bandia za uwanja huo, kumefanya mashabiki wa soka na wakazi wa Jiji la Mwanza kufurahishwa, kila mmoja akimwaga sifa kwa viongozi wa soka jijini Mwanza na TFF kwa jumla.
Pia wameimwagia pongezi kubwa Kampuni ya Mwananchi Communication LTD ambayo ilikuwa ni miongoni mwa wafuatiliaji wa karibu wa ukarabati wa ujenzi huo na kusaidia kupaza sauti mpaka mambo yalipokaa sawa.
Ikumbukwe kuwa mpango wa ujenzi wa uwanja huo unashirikisha Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
HALI YA SASA
Hali ya Nyamagana kwa sasa imekuwa kivutio kwani watu wamekuwa wakiutembelea kila mara kwa ajili ya kushuhudia ‘mkeka’ uliotandazwa eneo la kuchezea na kuzika kabisa kile kiwanja chakavu kilichozoeleka.
Kabla ya ujenzi kuanza, sehemu hiyo ilikuwa ni kama makazi ya watoto wa mitaani, ambao mara kadhaa walikuwa wakikutwa huko wamejitenga makundi. Pia uchafu uliokuwa umezagaa ikiwamo vinyesi, kwa sasa havionekani hataviongozi wa Chama cha Soka Mkoa, wanashinda ofisini kuhakikisha shughuli inakwenda sawa.
CHANGAMOTO
Licha ya ukarabati kuendelea kwa kasi, bado hofu ipo kwenye majukwaa ambayo yameharibika, huku paa lililoezuliwa mpaka sasa halijawekwa tena wala kuwa na jitihada za kurekebisha suala hilo.
Pia uzio wa uwanja bado ni tatizo, kwani uliopo kwa sasa unaonekana kuchoka kiasi cha kuruhusu wapita njia kuutumia kama chochoro yao ya kila siku.
Kadhalika ofisi za Chama cha Soka mkoani Mwanza (MZFA) na vyooni nako hakuko sawa wala kuridhisha, hivyo ni lazima wahusika waanze kuchukua hatua haraka kabla ya uwanja kuanza matumizi yake.
MZFA
Mwenyekiti wa MZFA, Jackson Songora anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana kuhakikisha uwanja huo unakamilika na kwamba watapambana hadi mwisho. Anasema mamlaka zinazohusika zihakikishe pia zinaboresha miundombinu ya uwanja huo ikiwamo kujenga ofisi na majukwaa.
Songora anasema kuwa MZFA watasimamia kadri iwezekanavyo ili kabla ya awamu yao ya utawala haijamalizika uwanja huo uwe umekaa sawa.
MIKAKATI
Katika ziara yake Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliwataka viongozi wa halmashauri kuhakikisha wanajenga majukwaa na kuweka hali nzuri ya uwanja.
Kutokana na agizo hilo, Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha anasema kuwa baada ya nyasi za bandia kuwasili na ujenzi kuanza, Jiji litahakikisha ukarabati wa majukwaa unafanyika mara moja.
Anasema walichokuwa wanasubiria zaidi ni vifaa vya ujenzi wa Uwanja huo, hivyo suala la majukwaa lazima lifanyike kwa haraka.
Anaeleza kwa sasa wanaendelea na vikao vya madiwani kupitisha bajeti na kwamba watakaa na Mkurugenzi kuhakikisha ujenzi huo unakamilika haraka iwezekanavyo.
“Tutakaa vikao na Mkurugenzi kuhakikisha bajeti inatengwa haraka na ukarabati unaanza, ili Nyamagana iwe ya kisasa na mwonekano mpya,” anasema Kotecha.
“Sisi tulitoa Sh200 milioni kwa ajili ya kufanikisha ujenzi unaofanyika huku fedha nyingine kama Dola 500,000 zikitolewa na Fifa, hivyo hatuna wasiwasi na majukwaa,” anaongeza.
Kotecha anawashauri pia wadau mbalimbali kuwekeza kwenye uwanja huo kwa kujitangaza na kuwa uwanja huo utakuwa na manufaa makubwa hapa mkoani na nchini kwa jumla.
WADAU WAFUNGUKA
Baadhi ya wadau wa soka jijini hapa wameonekana kufurahia hatua iliyofikiwa sasa ya ujenzi huo wa nyasi za bandia kwenye dimba la Nyamagana na kusema kuwa hadhi ya mkoa imerudi.
Kessy Mzirai ambaye pia ni Kocha Msaidizi wa Alliance FC, anasema uwanja huo awali umesaidia kuwatoa baadhi ya nyota wanaotesa kwenye soka la kitaifa na kimataifa.
“Hadhi ya Mkoa inarudi, kwa sababu uwanja huu wa Nyamagana, una faida kubwa sana, umewatoa wachezaji wengi wa kitaifa na kimataifa kama Joshua (Oscar), Ngassa (Mrisho), Tegete (Jeryson) na wengine,” anasema Mzirai.
Naye Hawa Bajanguo anasema kuwa hatua iliyofikia kwa sasa kwenye uwanja huo ni ya kutia matumaini na kwamba ni nafuu kwa klabu ambazo zilikuwa zikihangaika na viwanja.
“Hii ni faida kubwa hususani kwa timu ambazo mara nyingi zilikuwa zikihangaika, sasa hakuna tena kuhangaika, nashauri makandarasi wakamilishe haraka,” anasema Bajanguo ambaye ni Katibu wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa mwanza (TWFA).
PAMBA, TOTO KICHEKO
Aleem Alibhai, Mjumbe wa Kamati Utendaji wa klabu ya Pamba, anasema kurudi kwa uwanja wa Nyamagana katika kiwango cha juu, kumewafurahisha uongozi na timu nzima ya Pamba. Anasema yeye kama kiongozi atakuwa mstari wa mbele kushawishi kamati yao ndani ya timu kuiomba Bodi ya Ligi nchini kutumia uwanja huo kwenye mechi zao za Ligi Daraja la kwanza.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet anasema ni furaha kwao kuona Uwanja wa Nyamagana ukikamilika kwani wako tayari kuutumia kwenye mechi zao zozote hata kwenye mzunguko wa pili. Ameshauri Halmashauri kukarabati miundombinu ikiwamo vyumba vya kubadilishia nguo ili uwanja ukikamilika waweze kuutumia..
“Toto ni ya Nyamagana, hivyo itakuwa ni raha sana uwanja huo ukianza kutumika,” anasema Japhet.