Nyaishozi FC katika mtihani mzito kwa mashabiki Kagera

Muktasari:

  • Tangu Kagera Sugar ipande Ligi Kuu mwaka 2004, Mkoa huo ulipata timu moja ya daraja la pili, Kumuyange ambayo haikudumu na kupigwa bei, sasa macho na masikio ya wadau wa soka mkoani humo wameyaelekeza kwa Nyaishozi FC.

Mwanza. Hatma ya Mkoa wa Kagera kupata tena timu ya daraja la pili (SDL) itajulikana kesho Ijumaa Aprili 23, 2021 pale wawakilishi pekee mkoani humo, Nyaishozi FC itakapowakabili Copco Veteran ya jijini Mwanza katika mchezo wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa wa Mikoa (RCL).

Mchezo baina ya timu hizo unatarajiwa kupigwa uwanja wa Ilulu mkoani Lindi majira ya saa 8 mchana kisha saa 10:00 Temeke Squad na Baga Friends wakinyukana kusaka nafasi ya kupanda daraja la pili msimu ujao.

Hata hivyo mchezo huo unatarajia kuwa mgumu na wa ushindani kutokana na rekodi za wapinzani hao kutoka mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo Nyaishozi tangu waanze ligi hiyo hatua ya makundi hawajapoteza mechi yoyote wakishinda tano na sare tatu, huku Copco Veteran wakipoteza moja, na kushinda sita.

Mkoa wa Kagera una timu moja ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu tangu 2004, ambapo msimu wa 2019/20 walifanikiwa kupata Kumuyange FC, ambayo haikudumu hata msimu mmoja na kupigwa bei na sasa inajulikana kama Fountain Gate.

Nyaishozi yenye makazi yake wilayani Karagwe, imekuwa na matokeo mazuri tangu ianze kushiriki katika ligi hiyo ambayo ilishirikisha timu 28 na sasa zimebaki nne.

Afisa habari wa timu hiyo, Moses Richard amesema kutokana na ushirikiano uliopo kuanzia ndani na nje ya uwanja wanaamini timu hiyo itapanda daraja huku akisema sapoti na nguvu waliyonayo kutoka kwa wadau na viongozi mkoani humo inaongeza zaidi hamasa.

"Labda tushindwe sisi, lakini hatuna cha kulaumu kwa wadau wetu mkoani Kagera, kila mwenye uwezo ametusaidia na hata hapa kambini tunatembelewa na viongozi, wengine ni wa juu kwenye wizara hivyo kazi iliyobaki ni kwa vijana ndani ya uwanja" amesema Richard.