NMB, Yanga wazindua kadi za Kimataifa

Benki ya NMB kwa kushirikiana na Klabu ya Yanga, wamezindua kadi mpya maalum kwa  mashabiki wa timu hiyo.

Kadi hizo zinazotajwa kuwa na faida lukuki zinajulikana kama NMB YANGA Wolrd Debit maalum kwa mashabiki wa timu hiyo ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Miongoni mwa faida ya kadi hizo ambazo zinapatikana kwa  Sh 1milioni ni ni kufanya kazi katika ATM yoyote ulimwenguni.

Piaa shabiki atakayeinunua atapewa na  huduma nyingine kadhaa ikiwemo kupatiwa jezi  seti sita za Yanga.
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kadi uliofanyika Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, amesema: "Tumezindua kadi ya NMB Yanga World Debit (Black Card) ambapo ni kadi maalum yenye faida nyingi, unaweza kusafiri nayo ulimwenguni kote na kufanya malipo kokote katika ATM ambazo zinakubali master card.
 
"Ukisafiri unaweza kupata kukaa katika maeneo ya VIP Lounge katika viwanja vya ndege nje na ndani, pia unapata bima ya bure kwa kununua tiketi ya ndege kwa kupitia kadi hii.
 
"Katika bima hiyo unaweza kupata faida ya kulipwa fidia kama mizigo yako ikapotea ambapo utalipwa hadi Dola 3,000 (milioni 7), mizigo ikichelewa pia utalipwa hadi kiasi cha dola 300, pia kama utalipwa na bima hii pale ambapo ukinunua tiketi ya ndege kisha safari ikafutwa basi utalipwa hadi kiasi cha Dola 35,000 (milioni 20).
 
"Ukiwa na hii kadi pia unakua mteja wa NMB, ambapo utalipia baadhi ya mahitaji na pia kuna huduma ya Mkopo Mshiko Fasta ambao unamuwezesha mteja kukopa kiasi kuanzia 1000  mpaka 500,000.
 
"Pia kuna punguzo ambalo tunalifanya kila mwisho wa mwezi ambapo mteja kama ataenda sehemu za chakula akilipia kupitia NMB QR atapata hadi punguzo la asilimia 15," alisema Mponzi.
 
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema huo mwendelezo wa kukuza idadi ya wanachama wa Yanga.

"Katiba yetu inamtambua mwanachama ambaye anakuwa analipa ada yake ya uanachama shilingi 2,000 kila mwezi na kwa mwaka shilingi 24,000.
 
"Tunapongeza NMB kwa kuzindua kadi hii ambayo inawafanya wanachama kuwa wa hadhi ya juu kwa sababu tuliona kando ya mwanachama kulipia kadi anakuwa hapati kitu kingine zaidi ndiyo maana tukaja na kadi hii.
 
"Kadi hii kwa mwanachama wetu atakuwa analipia kiasi cha milioni moja, ambapo tumeweka hadhi kubwa katika kadi hii ambapo atapata jezi set sita, tiketi 10 za mechi katika eneo la VIP, pia atapata punguzo katika Hospital ya Agakhan kwa zaidi ya asilimia 10.
 
"Pia kutakuwa na huduma spesho kwa mwanachama ambaye atakuwa anamiliki kadi hii na pia kutakuwa na meneja mahusiano maalum ambaye atamletea huduma zake ofisini kwake.
 
"Tunataka kutengeneza thamani ambayo mwanachama ambaye atakuwa anatumia kadi hii aone kwamba kuna huduma zaidi ya kutumia kadi hii.
 
"Tunajua kwamba wanachama wanalipa kiasi cha 24,000 kama katiba yetu ambavyo inasema lakini hii ni maalum kwa ajili ya wanachama kulipia zaidi kwa ajili ya klabu yao na kiasi hicho cha milioni moja kitakuwa kwa mwaka mzima," alimaliza Hersi.
 
Baadhi ya wanachama ambao tayari wameshajipatia kadi hiyo ni pamoja na Isaac Chanji, Zamzam Sharif, Pindu Ruuyo na William Makoresho.
 
Ushirikiano huo wa Klabu ya Yanga na Benki ya NMB ulianza tangu Julai 2023 ambapo walianza kwa kuzindua kadi za uanachama maalum ambazo mbali na uanachama wao, pia zitawasaidia katika huduma nyingine za kifedha.
 
Mkataba wa makubaliano kati ya Yanga na Benki ya NMB, upo kwa kipindi cha miaka miwili ambapo Klabu ya Yanga ndani ya kipindi hicho, inatarajia kusajili zaidi ya wanachama milioni nane.
 
Ikumbukwe kwamba, kadi hiyo licha ya kumtambua shabiki na mwanachama wa Yanga, itaweza kumsaidia mwanachama wa timu hiyo kufanya miamala ya kifedha katika Benki ya NMB.