NJOHOLE: Akiri kucheza Ulaya kumempa kila kitu maishani-1

Njohole akiwa na mkewe Nadja na watoto wake, Aaron (mkubwa) na Elijah (mdogo)
Muktasari:
- Miaka 13 nyuma kumbe Simba ilimuuza Njohole kwa Dola 20,000 kwenda Yverdon pesa ambazo thamani yake kwa wakati huo ingeweza kuwa sawa au kukaribiana na kile ambacho Samatta aliuzwa.
NILITUA Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Geneva alfajiri ya Aprili 15 mwaka huu na kukumbana na baridi iliyopitiliza, kwangu ilikuwa ni balaa, lakini kwa wenyewe Wazungu ilikuwa baridi ya kawaida tu.
Nje ya Uwanja wa Ndege wa Geneva, mmoja kati ya viungo bora wa soka wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania mwishoni mwa miaka ya 1990, Renatus Njohole, ambaye pia alikuwa mwanafunzi mwenzangu wa darasa moja Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee jijini Dar es Salaam katikati ya miaka ya 1990, alikuwa ananisubiri.
Wakati Athuman Abdallah ‘China’ akichukuliwa kama mchezaji wa mwisho kutoka Tanzania kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa baada ya kina Sunday Manara, Kassim Manara, Aldolph Rishard na wengineo, Renatus Njohole alikuwa mchezaji wa kwanza wa kizazi kipya kwenda kucheza soka la kulipwa barani humo mwaka 1999 akitua Uswisi kuchezea timu ya Ligi Kuu, Yverdon. Nilimkuta Njohole katika urefu wake wa futi 6’0 akinisubiri nje ya uwanja wa ndege akiwa katika koti lililoashiria baridi kali. Alionekana mwenye siha njema na gari lake la kifahari aina Nissan Zafira liliashiria kuwa mambo yake ni mazuri.
Ni kama maji yanayofuata mkondo. Wakati kaka yake wa kwanza, Nicodemus Njohole alisifika kwa kutandaza kandanda safi uwanjani miaka ya 1980 na kisha kutokomea Austria kucheza soka la kulipwa, kaka yake mwingine, Deo Njohole ‘OCD” naye alicheza soka la kulipwa nchini Austria kabla ya kurudi Tanzania. Wakati tukiuacha uwanja wa ndege kuelekea katika mji anaouishi wa Yverdon kupitia Lausanne, ndipo Renatus anaanza kunieleza historia ya kusisimua ya maisha yake ya soka barani Ulaya ambayo imejificha kwa wengi.
“Karibu aisee. Nimekuwa Uswisi kwa zaidi ya miaka 13 sasa. Nilikuja hapa nikiwa mdogo tu wakati huo nilikuwa na miaka 19 nikitokea Simba ya nyumbani Tanzania. Hapa nilipo naongea Kifaransa zaidi ya Waswisi wenyewe,” anaanza kunisimulia Njohole huku akicheka.
Wakati mambo yakiwa magumu kwa wachezaji wa Kitanzania kwenda Ulaya nyakati hizo, Renatus anaelezea jinsi alivyopata zali la kucheza soka la kulipwa Ulaya, tena katika timu ya Ligi Kuu. Ilianza kama mzaha.
“Safari ilianzia kwa Mohammed Dewji ‘Mo’. Yeye ndiye sababu kubwa ya mimi kucheza soka la kulipwa Ulaya. Mara kadhaa alikuwa anakuja kufanya biashara zake hapa Geneva na ndio akaanza kusuka mipango kwa sababu wakati huo mimi nilikuwa nahodha wa Simba,” ananisimulia.
“Mo ndiye alimpa kazi wakala mmoja anayeitwa Remy ili anitafutie timu. timu ya kwanza iliyopatikana ilikuwa ya Ligi Kuu ilikuwa inaitwa Lausanne, ipo katika mji huo wa mbele yetu ambao tutaupita,” anasema hayo huku akiendesha gari kwa kasi. Mfumo wao wa uendeshaji magari unaruhusu kasi hiyo.
“Kocha wa Lausanne alinikataa bila ya kuniona uwanjani kwa sababu alisema nafasi zimejaa kwa wachezaji wa kigeni. Remy ilibidi anipeleke katika klabu ya Yverdon ambayo ilinikubali moja kwa moja baada ya kuniona mazoezini.
“Baadaye nilisaini mkataba wa miaka minne na Yverdon chini ya wakala wangu. Nikaanza mazoezi katika timu B ili niweze kuzoea mazingira kabla ya kupelekwa kikosi cha kwanza,” anasema Njohole.
Wakati Simba ikimuuza Mbwana Samatta kwenda TP Mazembe mwaka 2011 kwa kiasi cha Dola 100,000, kuna biashara ambayo Simba ilifanya kumuuza Njohole.
Miaka 13 nyuma kumbe Simba ilimuuza Njohole kwa Dola 20,000 kwenda Yverdon pesa ambazo thamani yake kwa wakati huo ingeweza kuwa sawa au kukaribiana na kile ambacho Samatta aliuzwa.
“Simba ilipata fedha kwa kuniuza. Niliuzwa kwa Dola 20,000 ambazo wakati huo zilikuwa nyingi. Aliyekuja kuchukua pesa alikuwa ni Katibu wa Simba wa wakati ule, Khalfan Matumla,” anaweka wazi Njohole.
“Alisafiri mpaka hapa Uswisi, akaja mpaka Yverdon. Timu yangu ilimtumia tiketi na ikampangia pia hoteli.”
Pamoja na kwamba Simba ilichukua fedha hizo, lakini inachekesha kwamba Njohole alilazimika kutoroka Dar es Salaam kwenda Uswisi kwa sababu ingekuwa vigumu kwa viongozi wa Simba kumruhusu kuondoka kwa wakati huo.
“Mimi ndiye nilikuwa nyota wa timu. Nilianza kuwika katika kiungo na wakati huo nilikuwa nahodha wa Simba kama ilivyokuwa katika timu ya vijana ya Tanzania.
“Hata hivyo katika safari hiyo ilibidi niondoke kimya kimya kwa kutoroka uwanja wa ndege na kuja huku kwa ndege ya Swiss Air kwa sababu nilijua kuwa viongozi wa Simba wasingeniruhusu.
“Nakumbuka Simba ile tulikuwa mimi, (Athuman) Machuppa, Prosper Omella, Musa Msangi, Will Cyprian, Juma Amir, Mohamed Mwameja, Athuman Machepe na wengineo. Hata hivyo ilibidi nitoroke kwa sababu nilijua Simba wangenikatalia.
“Nilipofika huku Simba wakajua kilichoendelea. Nilipopata timu ndipo viongozi wa Yverdon walipolazimika kufanya mawasiliano na Simba kwa ajili ya ITC (Hati ya Kimataifa ya Uhamisho), ndipo Matumla akaja,” anasema Njohole.
Wakati mazungumzo yetu yakiendelea, wakati huo tulikuwa tumeachana na mji wa Lausanne tukiingia katika mji mdogo wa Yverdon ambao Renatus alifikia kwa mara ya kwanza.
“Wakati huo Yverdon ilikuwa chini ya Rais wao mmoja aliyeitwa Cornu ambaye alikuwa tajiri sana. Huyu jamaa alikuwa anamiliki kiwanda cha biskuti. Timu ikaniweka katika hoteli nzuri inayoitwa La Prairie,” anasema Njohole.
Katika mechi zake za kwanza tu, Njohole alipata nuksi kubwa ambayo ilikaribia kuharibu maisha yake ya soka nchini Uswisi. Ni nuksi gani hiyo?
Itaendelea Jumanne ijayo…