Ni Simba na Yanga fainali

Monday January 11 2021
FINITE PIC
By Mwanahiba Richard

Nyota ya Miraji Athuman na Meddie Kagere imeendelea kung'ara kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo wameisaidia timu kuvuka hatua ya fainali ambapo sasa watacheza na Yanga Jumatano Januari, 13.

Yanga imefuzu kwenye nusu fainali ilipocheza na Azam FC na kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya matokeo ya dakika 90 zikimaliza kwa sare ya bao 1-1. Fainali hizo zitachezwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

FINITE PIC 1

Simba walipata ushindi huo wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo baada ya safu ya ulinzi kujichanganya na kuwapa mwanya nyota wa Simba kufunga.

Kagere ambaye ana mabao mawili kwenye mashindano haya ndiye alianza kutikisa nyavu za Namungo baada ya kipa Nourdine Balora kutoka golini hivyo kumpa kazi rahisi Kagere kufunga ikiwa ni dakika ya sita tangu kuanza kwa mchezo huo.

Miraji ambaye amefikisha mabao manne sasa na ndiye anaongoza kwa mabao kwenye mashindano hayo alifunga bao la pili dakika ya 40 akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na Francis Kahata.

Advertisement
FINITE PIC 2

Mwamuzi wa mchezo huo Mohammed Kassim Mohammed alitoa kadi ya njano kwa beki wa Namungo, Abdulrahiman Hudumu ikiwa ni dakika ya 26 ya mchezo baada ya kucheza rafu kabla ya Sixtus Sabilo kuinyima bao Namungo baada ya purukushani golini kwao na kujikuta mpira ukigonga mwamba na kutoka nje ya goli la wapinzani wao wakati tayari Beno Kakolanya akiwa amelala chini.

Namungo walipata bao la kufutia machozi dakika ya 87 likifungwa na Stephen Sey baada ya kumalizia kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Ramadhan Kichuya.

FINITE PIC 4

Kipindi cha pili, makocha wote walifanya mabadiliko ya vikosi vyao ambapo upande wa Simba, Seleman Matola aliwatoa Joash Onyango na kumuingiza Agele Coulibally pia alimtoa Taddeo Lwanga na kumuweka mshambuliaji Chris Mugalu.

Upande wa Namungo Fc, Hemed Morocco aliwatoa Idd Kipagwile na Jaffar Mohamed waliingia Blaise Bigirimana na Shiza Kichuya.

Katika mchezo huo, Mzamiru Yassin amechaguliwa kuwa mchezaji bora na kuzawadiwa Sh 500,000 kutoka kwa wadhamini wa mashindano hayo.

Kikosi cha Simba kilichoanza: Beno Kakolanya, David Kameta, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Joash Onyango, Taddeo Lwanga, Hassan Dilunga, yassin Mzamiru, Meddie Kagere, Francis Kahata, Miraji Athuman.

Namungo: Nourdine Balora, Haruna Shamte, Jaffar Mohamed, Stephen Duah, Idd Kipagwile, Hamis Khalifa, Abdulhalim Humud, Fredy Tangalo, Sixtus Sabilo, Stephen Sey na Erick Kyaruzi.

Advertisement