Mrithi wa Sven huyu hapa

MAKOCHA zaidi ya 100, walituma maombi ya kutaka kukikonoa kikosi cha Simba na tayari kati ya hao wamepigwa panga na kubakishwa kama 55 hivi ambao wataendelea kuchujwa ili kupata watano watakaopambana kupenya kumrithi Sven Vandenbroeck aliyetimkia Morocco.

Hata hivyo, kuna majina matatu ambayo mojawapo ni la mtu anayetajwa kuja kuvaa viatu vya Mbelgiji huyo aliyeitosa Simba ghafla na kuibukia FAR Rabat ya Morocco, ingawa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez amesisitiza hawataharakisha kuajiri kocha mpya hadi waendeshe mchakato wa kina kupata atakayewafaa na kuwapeleka mbele zaidi ya alipoachia Sven.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba leo itavaana na Namungo katika nusu fainali itakayopigwa usiku, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ataitisha kikao cha bodi ambacho kinaweza kufanyika kati ya Januari 15-20.

Katika kikao hicho ajenda kubwa zitakuwa mbili, usajili unaoendelea kushughulikiwa na ishu ya Kocha Mkuu wa kuchukua nafasi ya Sven ambaye atajadiliwa miongoni mwa majina matatu yanayopewa nafasi kubwa ya kulamba ajira Msimbazi.

Mwanaspoti limepata taarifa kutoka ndani ya Simba kuwa kuna majina 55 waliopenya katika orodha ya awali ya makocha zaidi ya 100 na wanatafutwa Tano Bora, lakini wanaopewa nafasi ni Kocha Msaidizi wa Raja Casablanca ya Morocco, Hicham Aboucherouane.

Hacham, ambaye ni msaidizi namba moja wa Kocha Mkuu wa miamba hiyo ya soka la Morocco Raja Casablanca, Jamal Sellami, huku mwingine anayepigiwa hesabu ni aliyewahi kuwa kocha wa vigogo wa soka Afrika, Al Ahly ya Misri, Rene Weiler aliyekiongoza kikosi hicho dhidi ya Simba katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2018-2019.

Weiler akiwa na Al Ahly amepata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri, Kombe la FA la Misri kabla ya kutimuliwa hivi karibuni kumpisha Pitso Mosimane kutoka Afrika Kusini.

Jina la tatu lililo kwenye rada za mabosi wa Simba kutoka miongoni mwa rundo hilo la orodha ya waomba kazi Msimbani ni Florent Ibenge anayeinoa timu ya taifa ya DR Congo na AS Vita waliopangwa nao kundi moja la A katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Inaelezwa, kwenye akili ya Mo Dewji ni kutaka kushusha kocha mwenye uwezo na (CV), kubwa si yule ambaye atakuja kutafuta mafanikio na Simba, kama ilivyokuwa kwa Sven.

Mmoja wa viongozi wa Simba, alisema hao makocha watatu, Hicham, Weiler na Ibenge wamefanya mazungumzo na uongozi ili kuona upatikanaji wao lakini dau lao ni pesa ndefu.

“Baada ya hapo kutakuwa na nyongeza pia ya wengine wawili ambao watafika idadi ya watano na siku ambayo bodi itakutana ndio watachuja na kubaki watatu ambao mmoja wapo ndio atakuwa kocha mpya wa Simba,” alisema.

“Ukiondoa makocha hao watatu mchakato bado unaendelea ili kuwajadili waliopo na kupitia CV zao ili kumchukua mmoja, ila kuna changamoto, Mo Dewji anatamka kocha mwenye uwezo huko alipotoka, lakini baadhi ya wajumbe wanamtaka atakayekuwa na njaa na kiu ya mafanikio.”

Simba itapaswa kujipanga ikiwamo kuvunja benki ili kumbeba Ibenge na hata Weiler kwani ni makocha wanaotajwa kuwa ghali na hii sio mara ya kwanza kwa kocha huyo wa DR Congo kuhusishwa na Simba, kwani hata kabla ya Patrick Aussems na Sven aliwahi kutajwa kuja.

Hata hivyo, Barbara akihojiwa juzi alisema, hawataharakisha kuchagua kocha ili kuhakikisha wanapata kocha sahihi, hawataki kukurupuka kisha mbele ya safari wajute, huku akisema baadhi yao wanatoka Serbia, Ufaransa, Ureno na baadhi ya nchi za Afrika, ila wanaendelea na mchujo.

“Bado tunaendelea kuchambua CV ili tupate kocha sahihi, kwani katika kuchagua, lazima uchukue muda kupata kocha sahihi kwa timu yetu. Ukiharakisha jambo utaharibu msimu mzima na mipango ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tumekusudia kufika mbali msimu huu,” alisema Barbara kuongeza;

“Tumeweka vigezo vya kumpata kocha sahihi ikiwamo uzoefu, leseni na vitu mbalimbali na lazima awe na uzoefu wa klabu wa miaka kuanzia mitano na hata katika timu ya taifa. Kuna CV kubwa mno na ndio maana tunataka muda wa kuzipitia kupata mtu sahihi.”

Kuhusu ishu ya usajili alisema wanaendelea kuwaangalia wachezaji wao watatu wanaojaribiwa katika Kombe la Mapinduzi, wakiwaridhisha watawasajili.

Wachezaji hao ni Wazimbabwe wawili, kiungo Ian Nyoni na beki Kevin Moyo pamoja na beki wa kati kutoka Uganda, Benard Agele.