Prime
Ngoma tatu nzito za Mzize

Muktasari:
- MSIMU wa Ligi Kuu Bara uko ukingoni, huku mashabiki wa soka wakisikilizia kujua utamalizikaje? Je ni ubingwa utatua mitaa ya Jangwani au Msimbazi? Zipi ni timu ambazo zitacheza mtoano kuwania kucheza na ile ya Championshipi ambayo ni Stand United?
MSIMU wa Ligi Kuu Bara uko ukingoni, huku mashabiki wa soka wakisikilizia kujua utamalizikaje? Je ni ubingwa utatua mitaa ya Jangwani au Msimbazi? Zipi ni timu ambazo zitacheza mtoano kuwania kucheza na ile ya Championshipi ambayo ni Stand United?
Sikia, wababe Simba na Yanga wako mzigoni leo katika viwanja viwili tofauti wakiwania ubingwa wa ligi hiyo, lakini nyuma yao kila mmoja anakabiliwa na kibarua cha kumrarua mwezake katika mchezo wa mwisho wa Dabi ya Kariakoo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Juni 25.
Wakati mambo yakiwa hivyo, kuna mambo matatu yanamkabili mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ambayo anapaswa kuyafanyia kazi hadi kufikia Juni 25 mwaka huu, siku ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.
Mzize ambaye huu ni msimu wa tatu anacheza Ligi Kuu Bara baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana ya Yanga, kwa sasa ana mabao 13, mawili nyuma ya kinara wa ufungaji wa ligi hiyo, Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye 15, pia yupo sawa na mshambuliaji mwenzake kikosini hapo, Prince Dube raia wa Zimbabwe.
Ukiangalia katika mechi tatu zilizobaki zenye jumla ya dakika 270, Mzize ana mtihani wa kwanza kuhakikisha anatwaa Tuzo ya Ufungaji Bora ambayo haijachukuliwa na mzawa misimu miwili mfululizo sasa tangu mara ya mwisho alipoibuka kinara George Mpole msimu wa 2021-2022 alipofunga mabao 17 akiitumikia Geita Gold.
Baada ya hapo, msimu wa 2022-2023 kinara alikuwa Mkongomani Fiston Mayele (Yanga) na Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ (Simba) ambao kila mmoja alifunga mabao 17, kisha 2023-2024 ikawa zamu ya Stephane Aziz KI (Yanga) raia wa Ivory Coast aliyefunga mabao 21.
Jambo la pili linalomkabili Mzize ni kufunga mabao manne ili yafike 17 na atafikia rekodi ya nyota mzawa aliyefunga mabao mengi kwenye ligi kwa kipindi cha misimu 10 iliyopita ambao ni, lakini akiongeza zaidi, yeye ndiye atashikilia rekodi hiyo.
Mwisho kabisa, Mzize analisaka bao lake la kwanza dhidi ya Simba kwani katika misimu mitatu sasa katika ligi, hajatikisa nyavu za Wekundu hao wa Msimbazi.
Katika misimu hiyo mitatu, Mzize amecheza Dabi ya Kariakoo tatu kwenye ligi ambapo ya kwanza ni ile ya Novemba 5, 2023 iliyomalizika kwa matokeo ya Simba 1-5 Yanga. Siku hiyo Mzize hakufunga, bali alitoa asisti mbili. Ya bao la tatu lililofungwa na Aziz KI na bao la nne lililofungwa na Maxi Nzengeli.
Baada ya hapo, akacheza Dabi ya Kariakoo nyingine ya Aprili 20, 2024 iliyomalizika kwa matokeo ya Yanga 2-1 Simba, hakufunga wala kuasisti. Kisha ya mwisho ni Oktoba 19, 2024, matokeo yalikuwa Simba 0-1 Yanga ambapo pia hakufunga wala kuasisti.
Mzize ambaye kwenye misimu mitatu ya Ligi Kuu Bara amefunga jumla ya mabao 24, timu alizozifunga ni Kagera Sugar (3), Polisi Tanzania (1), KMC (1), Geita Gold (1), Singida Big Stars (1), Coastal Union (1), Tanzania Prisons (2), Namungo (1), Azam (1), Mtibwa Sugar (1), Dodoma Jiji (3), Tabora United (2), Fountain Gate (3), KenGold (2) na Singida Black Stars (1).
DAKIKA 270 ZA KAZI
Katika mechi tatu zilizobaki zenye dakika 270, Yanga itaanza Jumatano hii kucheza dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kisha Juni 22, 2025 ni dhidi ya Dodoma Jiji, mechi ikipangwa kupigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kisha itamaliza dhidi ya Simba, Juni 25, 2025, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Duru la kwanza dhidi ya timu hizo ambapo Yanga ilishinda zote, Mzize alifanikiwa kufunga mabao mawili na moja dhidi ya Tanzania Prisons na lingine Dodoma Jiji, huku akishindwa kutikisa nyavu dhidi ya Simba. Kilichopo sasa ni kuendeleza alichokifanya awali na kuweka rekodi mpya ya kuifunga Simba.
MECHI 27, MAKOCHA WANNE
Mzize ndani ya kikosi cha Yanga, msimu huu ndiye mchezaji aliyecheza mechi zote 27 za Ligi Kuu Bara hadi sasa akitumika kwa dakika 1,678.
Katika mechi hizo 27, amesimamiwa na makocha wanne tofauti ambao ni Miguel Gamondi (10), Sead Ramovic (6), Abdihamid Moalin (1) na Hamdi Miloud (10).
MISIMU 10 YA WAZAWA
Ukiangalia wakati huu ambao Mzize anapambana katikati ya wageni kwenye kufunga mabao ndani ya Ligi Kuu Bara, kwenye misimu kumi iliyopita imeshuhudiwa mara nne pekee wazawa wamebeba tuzo ya ufungaji bora, huku iliyobaki ikienda kwa wageni.
Katika mara hizo nne, Simon Msuva ambaye kwa sasa anaitumikia Al-Talaba SC ya Iraq, amechukua mara mbili wakati anaichezea Yanga, ilikuwa msimu wa 2014-2015 alipofunga mabao 17 na 2016-2017 akifunga mabao 14 ambapo alilingana na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting ambaye naye ni mzawa.
Baada ya hapo, mzawa mwingine aliyebeba tuzo hiyo ilikuwa msimu wa 2020-2021 ambapo John Bocco alifunga mabao 16 alipokuwa Simba, kisha 2021-2022 ikawa zamu ya George Mpole aliyekuwa Geita Gold akifunga mabao 17.
Rekodi zinaonyesha, wazawa wamekuwa wakipigana vikumbo na wageni katika kuwania tuzo hiyo lakini mara kadhaa wanakwama.
Katika msimu wa 2014-2015, Msuva alitoka kidedea akifunga mabao 17, kisha 2015-2016, Elias Maguri aliyekuwa Stand United na Jeremiah Juma (Tanzania Prisons), kila mmoja alifunga mabao 15, wakati kinara wa jumla alikuwa Amiss Tambwe (Yanga) aliyefunga mabao 21.
2016-2017, ngoma ikarudi kwa wazawa pale Msuva na Abdulrahman Mussa walipomaliza na mabao 14 kila mmoja na kugawana tuzo ya ufungaji bora.
Msimu wa 2017-2018, mzawa aliyefunga mabao mengi alikuwa John Bocco (Simba) na Marcel Boniventure (Majimaji) ambao kila mmoja alipachika 14, huku kinara wa jumla akiwa Emmanuel Okwi (Simba) aliyefunga mabao 20.
Katika msimu wa 2018-2019, Salim Aiyee (Mwadui) alifunga mabao 18 na kuwa mzawa aliyemaliza na mabao mengi, huku kinara akifunga mabao 23 ambaye ni Meddie Kagere (Simba).
Msimu wa 2019-2020, wazawa waliofunga mabao mengi ni Yusuph Mhilu (Kagera) na Wazir Junior (Mbao) ambayo ni 13 kila mmoja, huku Kagere (Simba) akiwa tena mfungaji bora kwa kutupia 22.
Mabao 16 aliyofunga John Bocco msimu wa 2020-2021 akiwa Simba, yalimfanya kuwa kinara wa ufungaji na mzawa mwingine aliyefanya hivyo alikuwa George Mpole (Geita Gold) katika msimu wa 2021-2022 alipofunga mabao 17.
Bocco akiwa Simba, akafunga tena mabao 10 na kuwa kinara kwa wazawa msimu wa 2022-2023 wakati ambao Fiston Mayele (Yanga) na Saidi Ntibazonkiza (Simba) wakimaliza kileleni na mabao 17 kila mmoja.
Msimu wa 2023-2024, Feisal Salum akiwa Azam, alifunga mabao 19 na kuwa kinara kwa wazawa wakati mfungaji bora akiwa Stephane Aziz KI (Yanga) aliyefunga mabao 21.
ISHU YA UFUNGAJI BORA
Kwa sasa Mzize ana mabao 13 sawa na Dube, huku Ahoua akiwa nayo 15. Kama hadi mwisho wa msimu mambo yakimnyookea Mzize na kufungana mabao na Ahoua, maana yake Mzize atashinda tuzo hiyo.
Hiyo inatokana na kanuni za Ligi Kuu Bara toleo la 2024 zilivyo katika kipengele cha Vikombe na Tuzo.
Kanuni ya 11 inayozungumzia Vikombe na Tuzo, kifungu cha 13, kifungu kidogo cha 13.1, inasema: “Magoli yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatakuwa na alama mbili (2) na magoli yaliyofungwa kwa njia ya penalti yatakuwa na alama moja (1). Mchezaji mwenye alama nyingi atakuwa mshindi.”
Hivi sasa Mzize mwenye mabao 13 aliyonayo, hakuna la penalti, hivyo inamfanya kuwa na pointi 26, akiongeza mawili yasiyokuwa ya penalti yanakuwa 15 na kukusanya pointi 30. Mabao 15 aliyofunga Ahoua, sita ni ya penalti, hivyo kwa mujibu wa kanuni, jumla amekusanya pointi 24.
MWENYEWE ANASEMAJE
Kuhusu suala la kufunga, hivi karibuni Mzize aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Kufunga ndio kazi ya mfungaji, nami naona raha kila ninapoisaidia timu, kwa ishu ya Mfungaji Bora siwezi kuzungumzia, lakini kiu ni kuona Yanga inatetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.”