NBC yakabidhi zawadi kwa Bruno Gomes, kocha Pluijm
Mkuu wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu (kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya Sh1 milioni kwa mchezaji Bruno Gomes wa Singida Big Stars aliyetangazwa mchezaji bora wa ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League Januari 2023.
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambao ni mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League mwishoni mwa wiki ilikabidhi zawadi ya pesa na tuzo kwa mchezaji bora wa ligi hiyo wa mwezi Januari 2023, Bruno Gomes pamoja na kocha bora wa mwezi huo, Hans Van Pluijm wote kutoka Singida Big Stars.
Makabidhiano ya zawadi hizo yalifanyika muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo baina ya Simba SC dhidi ya Singida Big Stars uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mchezo ambao ulikamilika kwa timu ya Simba SC kuibuka na ushindi wa goli 3-1.
Alikuwa ni Mkuu wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu aliyekabidhi mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya Sh1 milioni, tuzo pamoja na kisimbuzi cha Azam kwa mchezaji Bruno Gomes huku pia Kocha Van Pluijm kutoka timu hiyo akipatiwa mfano wa hundi yenye kiasi kama hicho cha pesa, tuzo na kingamuzi cha Azam.