Nangu: Kumkaba Pacome, ufanye kazi muda wote

Muktasari:
- Beki huyo chipukizi ameliambia Mwanaspoti kuwa kiungo mshambuliaji huyo wa Yanga ni mchezaji mwenye kasi na akili ya kubadilisha mechi, jambo ambalo kwa beki yeyote anayemkaba anapaswa kufanya kazi ya ziada uwanjani.
JKT Tanzania imekwama katika mbio za kusaka tiketi ya michuano ya CAF baada ya kufungwa mabao 2-0 na Yanga katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), huku beki Wilson Nangu akisema kumkaba Pacome Zouzoua inahitaji umakini mkubwa.
Beki huyo chipukizi ameliambia Mwanaspoti kuwa kiungo mshambuliaji huyo wa Yanga ni mchezaji mwenye kasi na akili ya kubadilisha mechi, jambo ambalo kwa beki yeyote anayemkaba anapaswa kufanya kazi ya ziada uwanjani.
Pacome amefunga mabao tisa na asisti tisa katika Ligi Kuu, jambo ambalo Nangu mwenye mabao mawili amedai katika mechi walizocheza dhidi ya Yanga msimu huu amegundua namna ambavyo Pacome alivyo makini.
“Ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kufikiria nyakati awapo uwanjani, mfano mipira ya kufa ambayo beki anaweza akaidharau. Unaweza ukashtukia Pacome kashaufikia mpira na unaweza ukaleta madhara langoni, endapo hutamuwahi kumzuia,” alisema na Nangu.
“Kwa mechi tulizocheza na Yanga nililijua hilo, hivyo nikawa naongeza umakini wa kuhakikisha namkaba ili asilete madhara ya kufika langoni mara kwa mara.” JKT Tanzania katika mechi 28 imeshinda nane, sare 11, ikipoteza tisa, huku ikifunga mabao 27 na kufungwa 26, ikikusanya pointi 35, kitu ambacho Nangu alisema: “Tuna mechi mbili ngumu (dhidi ya Pamba na Mashujaa) zilizojaa hesabu kali, matamanio ni kumaliza nafasi ya tano.”